Habari Mseto

Mwili wa aliyejirusha baharini kutoka kwa feri wapatikana

November 26th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

MWILI wa mwanamume aliyezama baharini katika Kivuko cha Likoni, Kaunti ya Mombasa mnamo Jumapili baada ya kujirusha kutoka kwa Feri, MV Harambee hatimaye umeopolewa Jumanne.

Katika tarifa kwa vyombo vya habari Shirika la Hudma za Feri Nchini (KFS) limesema kwamba mwili huo umepatikana katika Kivuko hicho karibu na eneo la Feri ya Zamani.

Shirika hilo limesema kwamba vitengo mbalimbali vya wapigambizi vimefanikisha uopoaji wa mwili huo.

Mwili huo umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Chumba cha Kuhifadhi maiti cha hospitali ya Rufaa ya Coast General.

Shirika hilo limebainisha kwamba kufikia sasa hakuna mtu ambaye amejitokeza kusaidia kutambuliwa kwa mwili huo.

Mwanamume huyo aliyekuwa amevalia fulana nyeupe na suruali nyeusi alijirusha katika Bahari Hindi juzi usiku mwendo wa saa saba na nusu alipokuwa akivushwa na Feri hiyo MV Harambee kutoka ng’ambo ya Likoni kuelekea Kisiwani.

Ikumbukwe Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu walizama baharini walipokuwa wakivushwa na Feri iyo hiyo kutoka ng’ambo hiyo ya Likoni kuelekea Kisiwani mwishoni mwa Septemba.