Habari Mseto

Mwili wa Cohen wapatikana shimoni nyumbani kwake Kitisuru

September 14th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

MWILI wa bwanyenye Tob Cohen, aliyetoweka yapata siku 50 zilizopita ulipatikana Ijumaa katika shimo la maji-taka nyumbani kwake katika mtaa wa Kitisuru, Nairobi.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), George Kinoti alithibitisha kwamba maafisa wa upelelezi walipata mwili huo.

Bw Kinoti alisema mwili huo ulipatikana jana alasiri, siku moja baada ya mkewe Sarah Wairimu kufikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka ya kuua.

Alisema Cohen aliuawa kinyama baada ya kufungwa mikono na shingo kisha mwili wake ukatumbukizwa kwenye shimo.

“Tulifanya uchunguzi wa kina na tulipopata ripoti, kama wapelelezi tuliamua kufunga boma kama eneo la uhalifu na tumefaulu kupata mwili wa Cohen,” alisema.

“Cohen aliuawa kikatili ndani ya boma lake. Waliomuua ni watu katili sana,” alisema Bw Kinoti.

Alisema tayari wanawazuilia washukiwa wawili na watawakamata wengine. Bwanyenye huyo alikuwa akitafutwa tangu alipotoweka na wapelelezi walishuku mkewe alihusika na kutoweka kwake.

Mnamo Alhamisi, mahakama iliamuru kwamba akapimwe kubaini ikiwa ana akili timamu kabla ya kushtakiwa.

“Mwili huo ulipatikana ndani ya shimo la maji-taka nyumbani kwake,” Bw Kinoti aliwaambia wanahabari katika eneo la tukio alikofika huku akiandamana na wapelelezi kutoka kitengo cha kuchunguza mauaji.

Bi Wairimu ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji yake, pamoja na wakili wake, Philip Murgor, pia walikuwa katika makazi hayo pamoja na maafisa wa DCI.

Cohen ambaye aliwahi kuhudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Philips East Africa, ameishi Kenya kwa miaka mingi.

Uchunguzi wa hali kiakili

Bi Wairimu alifikishwa kortini mnamo Alhamisi lakini Jaji Charles Kariuki akaamuru kwamba kesi hiyo isikizwe mnamo Jumatatu wakati ambapo ripoti kuhusu hali ya kiakili ya Wairimu itawasilishwa ili jaji huyo aamue ikiwa anaweza kushtakiwa kwa mauaji.

Hata hivyo, Bw Murgor alilalamikia hatua ya kuahirishwa kwa kesi hiyo ikizingatiwa kuwa mteja wake amezuiliwa korokoroni muda wa siku 16.

Bw Murgor aliruhusiwa kuandamana na Bi Wairimu atapokuwa akichunguzwa akili kwani majuzi alidai kuwa maafisa wa upelelezi wanaochunguza kesi hiyo walimnyanyasa kimapenzi mteja wake.

Kesi hiyo sasa itatajwa mbele ya Jaji Jessie Lesiit mnamo Jumatatu.

Bi Wairimu alipokamatwa majuma mawili yaliyopita, Bw Kinoti alisema ndiye mshukiwa mkuu na ndio maana alikamatwa na wapelelezi walishuku Cohen aliuawa.

Kwenye mahojiano ya awali na maafisa wa polisi, inaripotiwa kuwa Bi Wairimu aliwaambia maafisa wa upelelezi kwamba Cohen alionekana mara ya mwisho mnamo Julai 20 alipoondoka nyumbani kwao Kitisuru, Nairobi na tangu wakati hakuonekana tena.

Kwenye barua aliyoandikia ubalozi wa Uholanzi, mwanamke huyo alisema kwamba Tob alikuwa akikabiliwa na tatizo la msongo wa kiakili ambalo lilikuwa likimsababishia matatizo mengi.