Mwili wa Magufuli kuwasili Dodoma Jumapili jioni

Mwili wa Magufuli kuwasili Dodoma Jumapili jioni

Na Sharon Sauwa, MWANANCHI

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania,  John Magufuli utawasili jijini Dodoma Jumapili jioni Machi 21, 2021 na utalala Ikulu ya Chamwino  na utaagwa katika uwanja wa Jamhuri Jumatatu Machi 22, 2021.

Akizungumza Jumamosi Machi 19, 2021 katika uwanja huo mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema mwili wa  Magufuli utawasili katika uwanja wa ndege Dodoma saa 10:00 jioni na  utapelekwa katika Ikulu ya Chamwino.

Amesema msafara wa gari litakalobeba mwili huo utapita barabara za Chako Chako, Nyerere, Bunge, Morena, Buigiri hadi Ikulu.

“Wananchi wote wa maeneo hayo mnaombwa kujipanga kwenye barabara hizo nilizozitaja ili kutoa heshima zetu za mwisho kwa mpendwa wetu,” amesema.

Amesema Jumatatu saa 12.00 asubuhi mwili utapelekwa katika uwanja huo kupitia barabara mpya ya Mfugale, Buigiri, Morena, Bunge, mzunguko wa mkuu wa Mkoa, Nyerere.

Amesema Jumatatu itakuwa siku ya mapumziko hivyo wananchi wataweza kujitokeza kwa wingi zaidi na shughuli hiyo itaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

“Maandalizi ya kupokea mwili na kuaga yapo katika hatua za mwisho, tumeimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma karibuni sana katika kutoa heshima za mwisho,” amesema.

Amesema Jumanne saa 12.00 asubuhi mwili utaondoka katika Hospitali ya Benjamin Mkapa saa 12:00 asubuhi kwenda Uwanja wa ndege wa Dodoma kuelekea Zanzibar ambapo wakazi wa Pemba na Unguja watakongamana katika uwanja wa Amani ili kuuaga mwili wa kiongozi wao.

Vilevile tarehe 24 wakazi wa Mwanza nao watapata fursa ya kuuona na kuuaga mwili wa rais Magufuli.

Mwili huo baadaye utasafirishwa hadi nyumbani kwa rais Magufuli huko Chato, Geita ambapo wakazi wa eneo hilo watapata fursa ya kuuona mwili wa mwana wao kwa mara ya mwisho .

Na ifikiapo Machi 26 basi mwili wa rais huyo utapatiwa mkono wa buriani na kuzikwa nyumbani kwake huko Chato.

You can share this post!

Diamond aeleza alivyoulizwa na Magufuli kuhusu siri ya baba...

DINI: Usitishwe na wanaokusema vibaya,vumilia, huwezi...