Habari MsetoSiasa

Mwili wa Moi kuwasili uwanja wa Nyayo saa nne asubuhi

February 10th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MWILI wa Rais wa zamani Daniel Arap Moi utawasili katika uwanja wa Nyayo, Nairobi kwa ibada ya wafu mwendo wa saa nne asubuhi Jumanne, serikali imetangaza.

Akiongeza na wanahabari Jumatatu jioni Msemaji wa Serikali Kanali Mstaafu Cyrus Oguna alisema milango ya uwanja huo itafunguliwa saa moja asubuhi na wananchi wanatarajiwa kuwa wameketi kufikia saa mbili za asubuhi.

“Kwa sababu tunatarajia takriban watu 30,000 kuhudhuria, tunawauliza Wakenya kuwa wameketi kufikia saa mbili za asubuhi kwa sababu milango ya uwanja wa Nyayo itafunguliwa saa moja asubuhi kesho (Jumanne),” akasema.

“Na mwili wa Rais Mstaafu Hayati Mzee Daniel Arap Moi utawasili uwanjani humo mwendo wa saa nne za asubuhi. Kwa hivyo, wananchi wanaombwa kuwa wameketi na kutulia kwa heshima ya rais huyo wa zamani,” Bw Oguna akaongeza.

Rais Uhuru Kenyatta na wageni mashuhuri kutoka humu nchini na ng’ambo pia watakuwa wamewasili kufukia saa nne za asubuhi.

Barabara yenye shughuli nyingi ya Uhuru Highway itafungwa kutoka makutano ya barabara ya Likoni road hadi mzunguko wa barabara ya University Way.

Vile vile wenye magari hawataruhusiwa kutumia barabara ya Aerodrome road kuanzia sawa na barabara ya Bunyala Road kuanzia saa kumi na mbili alfajiri.

Barabara hizo zitafungwa ili kuruhusu magari ya watu mashuhuri watakaohudhuria Ibada ya hiyo kufika katika uwanja wa Nyayo ambao umefanyika ukarabati.

Na nje ya Nairobi polisi watawazuia waendesha matrela kutumia barabara kuu ya Nairobi kwenda Eldoret kuanzia Jumanne hadi Jumatano. Hii itatoa nafasi kwa msafara wa magari ya kwenda Kabarak,Nakuru, kupita kwa urahisi.

“Kando na kufungwa kwa barabara, maafisa wa polisi watashika doria katika barabara husika ili kuwezesha magari kusafiri bila kutatizika,” akasema Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.

Marehemu Moi atazikwa Jumatano Februari 12 nyumbani kwake Kabarak, eneo bunge la Rongai, kaunti ya Nakuru katika mazishi ya kitaifa yatakayoandamanishwa na taadhima za kijeshi na kiraia.

Mzee Moi ambaye aliongoza Kenya kama Rais wa pili kwa kipindi cha miaka 24 alifariki mnamo Febrauri 4, 2020 katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akipokea matibabu kwa miezi minne.