Habari Mseto

Mwili wa msichana aliyekwama kwenye mgodi wa dhahabu bado haujapatika siku tano baadaye

January 22nd, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

MWILI wa msichana mwenye umri wa miaka 15 ambaye alikwama kwenye mgodi wa dhahabu katika kijiji cha Narworwo, Lokesheni ya Alale, Pokot Kaskazini bado haujaondolewa siku tano baadaye.

Mwathiriwa, Nakiru Ngolenyang alikumbwa na mkasa huo Jumatano, Januari 17, 2024.

Hofu inaedelea kuwakumba wakazi wa eneo hilo kutokana na mwili huo kukosa kuondolewa kwenye mgodi.

Akiongea na wanahabari, afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Alale Geoffrey Ndiwa ambaye alikuwa eneo la mkasa akiongoza juhudi za uopoaji alisema kuwa Jumatano, kikundi cha akina mama kilikuwa kwenye eneo la mgodi kabla ya kuanguka huku wakiponea kifo chupuchupu.

Bw Ndiwa anasema akina mama hao baadaye waligundua kuwa msichana mdogo ambaye alikuwa ameandamana nao hakuwepo.

“Baada ya kugundua kuwa msichana alikuwa amefunikwa na udongo, tuliarifu wahusika wakiwepo kikosi cha kukabiliana na majanga cha kaunti,” alisema Bw Ndiwa.

Kikosi cha kupambana na majanga kwenye kaunti bado kinajaribu kuusaka mwili wa msichana huyo lakini haujapatikana.

Afisa wa kusimamia majanga katika kaunti hiyo David Chepelion alisema kuwa idara hiyo itapiga kambi katika eneo la mkasa hadi mwili huo uondolewe.

Bw Chepelion hata hivyo aliwaonya wakazi dhidi ya kuhusika kwenye shughuli hatari kama uchimbaji migodi ambazo zimekuwa zikiua wakazi kwa muda mrefu katika hali isiyoeleweka.

“Tunahitaji mashini ya kutusaidia kuondoa mwili huo,” alisema.

Emanuel Domong’ole, mzee wa mtaa alisema kuwa kuna harufu kutoka kwa shimo hilo lakini mwili haujaonekana.

“Mamake marehemu alijifungua na msichana huyo ndiye alikuwa analisha familia. Kuna shida ya njaa eneo hili,” alisema.

Chifu wa Lokesheni ya Alale Jackson Lokwakile alisema kuwa wazazi wanalazimika kupambana na hali ngumu ya maisha wakisaka mbinu mbadala za kujikimu sababu soko la mifugo limefungwa.

“Hawana pa kuuza mifugo ili wanunue chakula. Lazima wachimbe migodi ili wapate chakula. Shida kubwa wengi wao wanafunikwa kwenye migodi. Ni hatari sana hasa kwa watoto wadogo,” alisema.

Aliitaka serikali kuu kusambaza chakula kwa familia ambazo zimeathirika na baa la njaa.

“Wakazi wanakumbwa na wakati mgumu. Hawana chochote cha kula na kulisha familia zao pana,” alisema.

Alisema kuwa watu wengi wa eneo hilo wanakumbwa na uhaba wa chakuka suala ambalo limewasukuma kuenda kusaka dhahabu kwenye migodi.

“Wanauza dhahabu kupata pesa za chakula. Hali ngumu ya maisha imeathiri wakazi wote. Hakuna shule, ndio watoto wengi hutumia muda wao kwenye migodi,” alisema.

Familia na wakazi bado wamepiga kambi eneo la mkasa kwa siku tano sasa bila mafanikio ya kuondoa mwili huo.

Wakazi ambao waliongea na vyombo vya habari walisema kuwa eneo la mkasa limekuwa hatari kwa waokoaji sababu wameshindwa kuondoa matope na hata mawe kwenye migodi hiyo.

Hadi sasa, zoezi hilo linaendelea huku uwezakano wa kupata mwili huo ukiwa finyu haswa bila vifaa maalum.

Wakazi wengi wa eneo hilo wanakumbwa na uhaba wa chakula suala ambalo huwasukuma kwenye migodi kusaka fedha za kununua chakula.

[email protected]