NA RUTH MBULA
NAIBU Jaji Mkuu, Bi Philomena Mwilu, ameonya watu wanaoendeleza utamaduni wa ndoa za mapema kuwa watachukuliwa hatua wakinaswa.
Alisema kuwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18 hafai kuozwa kwa kuwa hatua hiyo inakiuka Sheria ya Watoto.
Jaji Mwilu alitoa wito kwa jamii zinazoendesha tamaduni hizo potovu kukoma akisema kuwa mtu atakayepatikana hatasamehewa.
Akizungumza katika Kaunti ya Narok, aliitaka jamii kuwa makini na kupiga ripoti yoyote inayohusiana na tamaduni hiyo potovu.
“Jamii inafaa kushirikiana na taasisi zinazowalinda watoto ili kudhibiti ndoa za mapema. Tunafaa kuwalinda watoto hasa wasichana dhidi ya ukeketaji, dhuluma za kimapenzi na ndoa za mapema,” akasema Jaji Mwilu.
Alisema ushirikiano wa karibu kati ya jamii na taasisi zinazopigania haki za watoto utasaidia kudhibiti desturi kama hizo nchini.