HabariSiasa

Kesi dhidi ya Jaji Mwilu yasitishwa

August 29th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MAHAKAMA Kuu Jumatano imesitisha kesi dhidi ya Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na wakili Stanely Kiima ambapo walishtakiwa kuhusika kwa ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi, baada ya kukamatwa na maafisa wa upelelezi katika ofisi yake Jumanne jioni.

Kesi hiyo sasa itaendelea Ijumaa. Jaji Chacha Mwita amesema kuwa kuna masuala ya kikatiba ya kuangaziwa hasa kukuhusu kukamatwa kwa jaji.

Bi Mwilu alifika na mawakili tajika, wakiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, James Orengo, Okong’o Omogeni kwenye mahakama ya kusuluhisha kesi za ufisadi Milimani, Nairobi.

Jaji Mwilu alipopelekwa kwa seli za mahakama wakati kesi ilisimamishwa kwa dakika 20 ili ipate fursa ya kutoa mwelekeo Agosti 29, 2018. Picha/ Richard Munguti

Mawakili wengine kama John Khaminwa, Harun Ndubi na Edward Waswa walio na sifa ya kuangusha kesi kubwa kubwa aidha wamo kwenye orodha ya wawakilishi wa Bi Mwilu, wakiibua hisia kuwa kutakuwa na vita vikali kortini.

Bi Mwilu alikamatwa Jumanne baada ya gazeti la Daily Nation kuchapisha habari kuu kuwa kungekamatwa jaji mkubwa nchini, akituhumiwa kushiriki ufisadi na kutumia mamlaka ya ofisi yake visivyo.

Jumanne, wanachama wa tume ya kuwaajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama (JSC), akiwemo Bi Mwilu walifanya kikao cha muda asubuhi huku kiongozi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji akifika katika mahakama hiyo ya juu Zaidi mara mbili.

Mkuu wa kitengo cha upelelezi (DCI) George Kinoti aidha alifika kwenye mahakama hiyo, kabla ya Bi Mwilu kukamatwa na maafisa wa DCI na kufikishwa kwenye afisi za DPP.

Jumatano asubuhi, wakili wa Bi Mwilu Okong’o Omogeni alishindwa katika juhudi zake za kuwataka DPP Haji na DCI Kinoti kuwasilisha kesi ya Bi Mwilu kwa JSC kutatuliwa huko.