Habari Mseto

Mwimbaji wa Injili akosolewa kwa kutoa wimbo wa ‘Yesu Ninyandue’

February 16th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

PASTA William Getumbe ambye pia ni mwimbaji wa Injili, amekosolewa vikali na wanamitandao kwa kutoa wimbo mpya wa ‘Yesu Ninyandue,’ wakimtaja kukosa maadili kwenye jamii.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya simu, mwanamuziki huyo ambaye ni baba wa watoto wanne amesema kutumia neno ninyandue ni kutokana na kizazi cha sasa kinavyotumia lugha ya Sheng, akitaka ujumbe wake kueleweka.

“Pasta wenzangu wamenikosoa kwa kutoa wimbo huu. Wananikosoa kwa njia nyingi kutokana na kiwango cha jinsi anaelewa ujumbe,” alisema Bw Getumbe.

Bw Getumbe alifafanua anavyoelewa neno ninyandue.

“Siku hizi hakuna Injili ya kubembeleza ama ya kuomba. Huo muda umepitwa na wakati. Injili ya sasa ni ya kuimba ujumbe wako ueleweke kutokana na kizazi cha sasa. Vijana mtaani hutumia neno ‘ninyandue’,” alianza kujitetea.

“Binafsi nilitumia neno hilo ikiwa na maana kutolewa chini kwenda juu. Kizazi cha kisasa sio cha kutumia lugha ya kubembeleza,” alikamilisha Pasta huyo.

Mwimbaji huyo aliye na cheti cha kutoa ushari wa saikolojia, alisema kutumia neno ‘ninyandue’ ni kivutio kwenye wimbo huo.

Wimbo huo uliopakiwa February 13, 2024, ulivutia hisia kutoka kwa Wakenya wakitaka Bodi ya Hakimiliki ya Muziki Kenya kupiga marufuku wimbo huo.

Baadhi ya maneno aliyotumia ikiwa ni  ‘Yesu ninyandue nipate mimba, Umekubali kunyaduliwa? Yesu ninyadue nipate maji ya uzima’.

Wanamtandao wanasema mwanamuziki huyo anatafuta umaarufu kwa njia isiyo sawa.

“Upuzi na upumbavu wa kutafuta umaarufu na tamaa,” alichangia Selina Guya.

Waikwa Maina alishangaa iwapo muziki huo upo kwenye kiwango cha ukristo.

“Huu wimbo utafanya ukristo kuwa na sura mbovu kwa niaba ya bwana wao mwenye nguvu,” alisema Waikwa Maina.

Mapema mwaka jana alikosolewa na wanamitandao kwa kuvalia diaper tupu na kuzunguka katika mji wa Eldoret na Kakamega wakati wa kutoa hamasisho la unyanyapaa unaoandama wazee wanaotumia sodo hizo.