Habari za Kitaifa

Mwindaji ageuka mwindwa: Afisa wa DCI akamatwa akiitisha hongo

April 10th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

AFISA wa Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) Jumatano, Aprili 10, 2024, alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kuitisha hongo ya Sh10, 000 kutoka kwa raia wa kawaida Nyandarua.

Kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), EACC ilisema mwathiriwa alikuwa ametafuta usaidizi wa afisa huyo ili aokoe Sh115, 000 zilizoporwa na matapeli kutoka kwa akaunti yake ya M-Pesa.

Kulingana na tume, mshukiwa (afisa wa DCI) alimwambia mwathiriwa kuwa ilikuwa ni lazima atoe hongo ili kuwezesha msako dhidi ya matapeli hao.

Afisa huyo ambaye jina lake lilitambuliwa kama Luke Nyasangah anahudumu katika kituo cha polisi cha Ngano, Kaunti Ndogo ya Kipipiri, Nyandarua.

Anazuiliwa katika korokoro ya kituo hicho akisubiri kuwasilishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuitisha hongo kinyume cha Sheria ya Maadili na Uongozi wa Maafisa wa Umma ya 2013.

Tukio hilo linajiri wiki moja tu baada EACC kutoa ripoti inayoonyesha kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ni mojawapo ya asasi za serikali kuu ambazo ni fisadi zaidi.

Kulingana na ripoti hiyo, idara hiyo ni miongoni mwa zile ambazo sharti Mkenya atoe hongo kabla ya kupewa huduma za umma ambazo kwa msingi zinapasa kutolewa bila malipo.

Tukio hilo la Nyandarua pia linajiri mwezi mmoja baada ya afisa wa cheo cha juu katika kampuni ya usambazaji nguzu umeme za nchini (KPLC) kukamatwa katika Kaunti ya Kwale kwa madai ya kuitisha hongo ya Sh10, 000 kutoka kwa mteja wa shirika hilo ili amuunganishie stima.