Habari Mseto

Mwingereza aliyejijengea boma Kakamega azikwa

July 13th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI na BENSON AMADALA

KISA cha Mwingereza aliyejijengea boma Kakamega lakini akaanza kupitia hali ngumu mara baada ya mkewe Mkenya kumsaliti na kumtema kimeibua hisia mbalimbali mitandaoni.

Barry Humber aliyewahi kuwa mkwasi wa kutajika na ambaye mazishi yake yamefanyika Jumamosi baada ya kufariki wiki moja iliyopita, alikuwa anamiliki kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 30.38 katika Kaunti ya Kakamega.

Pengine hakujua masaibu yaliyomsubiri alipotua nchini Kenya miaka 43 iliyopita jinsi alivyowahi kusimulia hapo awali.

Wakati wa uhai wake aliwahi kusema alikuja Kenya akidhamiria kukaa kwa muda wa mwaka mmoja huku akifanya kazi ya ujenzi pamoja na kuendesha shughuli za umisheni miongoni mwa jamii ya Wamaragoli.

“Ombi langu lilikuwa kukaa Kenya kwa mwaka mmoja tu. Rais akanieleza, Barry Humber nimesikia mengi kukuhusu, tafadhali ishi huku,” alisema Humber ambaye alikumbana na mauti akiwa na umri wa miaka 80.

Humber alikubali wito wa aliyekuwa Rais, Mzee Jomo Kenyatta na kuanza kuwasaidia wanajamii wa Maragoli kuhusiana na masuala ya ujenzi kwa kutumia ujuzi na maarifa yake ya kielimu.

Zama hizo mambo yalimwendea vizuri kiasi cha kukubali kugeuza uraia wake wa Uingereza na kuwa raia wa Kenya.

“Makamu wa Rais wakati huo, Daniel Moi alimweleza Rais Jomo Kenyatta: Hapa tuna mtu hapa anayetuelewa na anayeweza kufanya mambo ambayo tumekuwa tukitaka kufanya kwa muda mrefu,” alisimulia.

Ndoa

Maadamu alikuwa tayari amejipatia jiko, Humber hakuwa na wasiwasi wowote.

Alirudi kwao Uingereza ambapo aliuza mali yake yote, akarejea na kuanza kuishi rasmi nchini Kenya mnamo 1978.

Kazi yake ya ujenzi wa hospitali eneo la Magharibi mwa Kenya ilibobea huku akipata usaidizi kutoka kwa mataifa mengine ya ulaya kama vile Denmark, Ujerumani, na Finland.

Alinunua ardhi na kwa kuwa hakuwa amepata uraia wa Kenya, akaandikisha mali yake kwa jina la mkewe waliyekuwa wamefunga nikaha.

“Nilinunua ekari 30.3 za ardhi na kuziandikisha kwa jina la mke wangu kwa sababu sikuwa raia wa Kenya. Tulifanya harusi hadharani kila mtu akiwa na ufahamu wa kile kilichokuwa kikiendelea kati yangu na mke wangu,” alisema.

Hata hivyo, masaibu yake yalianza siku moja mke wake alipoamua kumtema, akauza mali yao yote na kutoweka na mwanamume mwingine.

“Niliishi katika hoteli ya HighView mjini Kitale kwa mwaka mmoja kwa sababu sikuwa na pa kwenda,” alieleza.

Licha ya kupata hakikisho kutoka kwa aliyekuwa Rais Daniel Moi – ikiwa imepita miaka kadhaa tangu alipokuwa ni makamu wa Rais – Humber alihangaika kwa muda wa miaka 13 bila kupata usaidizi wowote kutoka kwa polisi; wa kutaka arejeshewa mali yake.

Alilazimika kuuza ardhi yake ya ekari 12 ili kulipa mkopo aliochukua mke wake na kujivinjari na mume mwingine licha ya kwamba walikuwa na watoto watano wa kambo.

Humber amefariki akiwa hana mtu wa kumtegemea nyumbani kwao Uingereza ila nduguye kwa sababu watu jamaa yake yote walikwisha aga dunia.

“Sina familia isipokuwa kakangu mdogo tu ambaye anajihusisha na masuala ya elimu,” alisema Humber ambaye mwanawe ni mwendeshaji wa bodaboda mjini Kakamega ambaye kipato chake ni cha chini.