Mwingine afungwa miaka 24 jela kwa ufisadi

Mwingine afungwa miaka 24 jela kwa ufisadi

Na RICHARD MUNGUTI

VITA dhidi ya ufisadi vilipamba moto Jumanne baada ya korti jijini Nairobi kumfunga gerezani miaka 24 meneja wa kampuni ya umma kwa kosa la kupokea hongo ya Sh910,000.

James Ambuso Omondi alisukumwa jela siku moja tu baada ya aliyekuwa meneja wa masuala ya uwekezaji katika Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), Francis Zuriels Moturi kufungwa miaka 14 ama alipe faini ya Sh2.4 bilioni kwa ufujaji wa Sh1.2 bilioni.

Ambuso, ambaye alikuwa meneja masuala ya fedha na usimamizi katika Mamlaka ya Kusimamia Rasilmali za Maji (KWRMA) anaweza kuponyoka jela iwapo atalipa faini ya Sh7.6 milioni.

Akitoa hukumu dhidi ya Ambuso, hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi ya Milimani jijini Nairobi, Bi Esther Nyutu alisema Ambuso alipatikana na hatia ya kuitisha na kupokea hongo ya Sh445,000 kutoka kwa meneja wa mamlaka hiyo katika jimbo la Mombasa, Bw Geoffrey Mworia.

Pia alipokea hongo ya Sh465,000 kutoka kwa Bw Boniface Mwaniki aliyekuwa akisimamia eneo la Tana.

Hakimu alisema mashahidi 16 walieleza korti jinsi Ambuso alikuwa akiwapigia simu wampe hongo ili aendelee kufadhili miradi katika maeneo wanayosimamia na pia asiwahamishe.

Walalamishi walikuwa wakituma hongo hizo kwa nambari ya simu ya MPesa ya mshtakiwa kati ya 2012 na 2013.

Alipewa siku 14 kukata rufaa.

  • Tags

You can share this post!

Mizozo ya uwaniaji vyeo yatishia umoja wa ‘Kenya Kwanza’

CECIL ODONGO: Ni kinaya Mudavadi kusaliti OKA ilhali...

T L