Bambika

MWISHO WA LAMI? Size 8 atangaza kuachana na DJ Mo, mashabiki hawaamini

Na SAMMY KIMATU August 3rd, 2024 1 min read

MWANAMUZIKI maarufu nchini Kenya wa nyimbo za injili Linet Munyali, almaarufu Size 8, ametangaza mwisho wa ndoa yake na mumewe DJ Mo, jambo lililoibua hisia kali miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Size 8 kwenye posti yake kwenye mtandao wa Instagram Alhamisi aliandika kwamba anaanza ukurasa mpya wa maisha kama mwanamke asiye na mahusiano na wanaume.

“Wakati mwingine ndoa huwa imara katika neema ya Mwenyezi Mungu na wakati mwingine pia ndoa husambaratika, hata hivyo Mungu ndiye Mkuu,” akaandika.

Aliandika kwamba ameolewa kwa miaka 11 lakini kuanzia sasa yeye hana mume.

“Nilikuwa kwenye ndoa kwa miaka 11 lakini kuanzia sasa mimi ni mwanamke hana mume,” akaandika.

Aliendelea kusema katika ukurasa wake kwamba ana imani na matumaini kwamba Mungu ndiye anayeongoza maisha yake na licha ya hayo, anamtukuza Maulana.

Mashabiki na wafuasi wa mitandao ya jamii wameachwa vinywa wazi kufuatia tukio hilo kwa sababu siku nne zilizopita Size 8 alikuwa ameweka picha kwenye Instagram akiwa na Dj Mo.

Katika picha hiyo mtandaoni, Size 8 aliandika, “Mtu anaweza kufuata au kukimbiza elfu moja lakini wawili wanaweza kufukuza au kukimbiza elfu kumi katika jina la Yesu.”

Wakenya walipokea habari hizo kwa hisia tofauti huku baadhi yao wakihoji kwamba hizi ni sarakasi za wasanii na kufananisha tukio hilo sawa na lingine lililokuwa la msanii Bahati na mkewe Diana Marua.

Vilevile, wafuasi wa wasanii hao wanahisi hizi ni mbwembwe za wawili hao na kwamba huenda wamewafichia kadi na kusema huenda wawili hao wako karibuni kuchomoa kibao cha muziki.