Makala

MWITHIGA WA NGUGI: Viongozi waunganishe Wakenya si kuonyeshana ubabe

January 25th, 2020 2 min read

Na MWITHIGA WA NGUGI

TANGU kushuhudiwa kwa salamu za kheri kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ama kweli kuna mabadiliko si haba yameonekana.

Mwanzo tuliona kuzaliwa kwa jopo la kujenga madaraja na uwiano almaarufu BBI, jambo ambalo kama muujiza joto la kisiasa lililokaribia kuliteketeza taifa letu lilipungua na mwanzo mpya wa majadiliano kati ya mahasimu wakuu wa kisiasa ukabadilisha taswira nzima ya taifa letu.

Tangu hapo tulipata utulivu nchini jambo ambalo liliwapa matumaini makubwa Wakenya ya kuwa na taifa moja lenye uwiano na pia lenye mazingira bora ya kuwekeza na kufanya biashara.

Hata hivyo, sio kila kitu king’aacho huwa ni dhahabu, hata kama viongozi wengi wa mirengo tofauti ya kisiasa wamejitokeza bayana na kuonyesha nia yao ya kuunga mkono ripoti ya BBI, hapa na pale kumejitokeza hali ya mshikemshike ya kisiasa huku baadhi ya viongozi wakionekana kutumia kila kikao cha kuhamasisha umma juu ya BBI, kuingiza siasa za mirathi ya uchaguzi wa mwaka 2022, hali ambayo inaonekana badala ya kuliunganisha taifa kama ilivyotarajiwa hapo awali sasa hilo linatia nyufa na migawanyiko.

Huu si wakati wa kampeini za 2022, wala wakati wa kuwapangia viongozi viti katika serikali ijayo na wale wanaofanya hivyo na wakumbushwe kuwa Wakenya wamegutuka na wanajua wanachotaka kutoka kwa jopo hili la BBI na yeyote yule hafai kutumia wakati huu kujitafutia makuu ya kibinafsi.

Sikatai kunayo haja ya kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kujenga madaraja na uwiano kati ya wananchi, lakini hiyo mikutano ya uhamasisho kamwe haifai kutumiwa na wanasiasa kuwadhalilisha viongozi wengine kadamnasi ya halaiki.

Wakenya wanachohitaji zaidi ni kusikia kuhusu zile ajenda tisa zilizopo kwenye ripoti hii ya BBI na jinsi ajenda hizi zitakapotekelezwa zitakavyoyaboresha maisha ya Wakenya na kutuepushia vurugu na zahama kila baada ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Wakenya tusisahau wangali wanakabiliwa na matatizo mbalimbali, vijana wengi hawana kazi, umasikini unawaponza wengi na vile vile saratani ya ufisadi ingali ni kizingiti kikuu kwa maendeleo ya taifa. Na wengi wanachotaka kuona na kusikia ni suluhu ya matatizo kama haya badala ya siasa za malumbano.

Si vyema kuendelea kusikia tetesi na minong’ono kila baada ya miaka mitano, eti kulikuwepo na wizi na udanganyifu kwenye uchaguzi. Hebu na tuone serikali na wanaobuni sera wakija na mikakati ya kubuni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itakayokubalika na wote.

 

[email protected]