Makala

MWITHIGA WA NGUGI: Wazazi watimize majukumu yao kwa watoto kikamilifu

January 18th, 2020 2 min read

Na MWITHIGA WA NGUGI

KADRI siku zinavyozidi kusonga ndivyo mambo mengi yanavyozidi kubadilika.

Tofauti na miaka ya hapo awali, ulezi wa watoto unaonekana tayari umechukua mkondo mpya.

Katika enzi zetu mtoto alichukuliwa kuwa mali ya jamii; aliyekosea alijua bayana kwamba angeweza kuadhibiwa na mzazi yeyote yule katika jamii na hilo lilihakikisha kukuzwa kwa hulka njema kwa watoto wote.

Shuleni pia, hakukuwepo na tofauti kwani kiboko kilitembezwa kwa wote na hakuna aliyelalamika, kwani ni hicho kiboko kilichotufanya kufuata sheria za shule, kuwaheshimu walimu na kutunyoosha kimaadili.

Tofauti na leo ni kwamba kwa upofu wetu wa kujitwika usasa na kiburi cha tetesi za kuzijua haki zetu, walimu walipokonywa kiboko shuleni. Walichoachiwa nafasi ya kuwapigia watoto watundu kelele tupu hata wanapokuwa tishio kwa maisha yao.

Ni hivi majuzi tu taifa hili lilipoweza kushuhudia tukio la kusikitisha katika Kaunti ya Kitui, ambapo wazazi walimshambulia mwalimu mmoja wa kike, waliyempiga na hatimaye kumteketeza kwa madai eti shule aliyosimamia ilifanya vibaya kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mwaka jana. Ama kweli huu ni uhayawani ulioje?

Badala ya kutafuta suluhu kama jamii, tunaonekana kuwalimbikizia lawama walimu wetu pasi kwanza kuangalia ni wapi kama wazazi, tulipoPOtezea dira ya ulezi.

Kwangu mimi lawama za kwanza zimo mikononi mwa wazazi.

Kuanzia kiamboni wazazi wamefeli mtihani wa ulezi. Wazazi wengi kila siku wamo mbioni kusaka hela usiku na mchana, na hata baadhi yao hawapati hata dakika moja ya kukaa na watoto wao na ndiposa wengi wameliachia jukumu la ulezi wa watoto wao mikononi mwa vijakazi na walimu.

Kwa miaka kadhaa, nimekuwa nikihudhuria mikutano ya shule na hasa wakiwemo wazazi na kile ambacho nimeshuhudia wazi ni kutowajibika kwa wazazi. Wengi hata huwa hawana muda wa kuwepo mikutanoni ili angalau wajulishwe juu ya maendeleo ya shule na changamoto zilizopo.

Hii basi ikiwa ndiyo taswira kamili ya shule zetu, tunatarajia matokeo gani? Tusipokuwa na ushirikiano mwema kati ya wazazi, walimu na wanafunzi tusijidanganye kuwa tutapata matokeo mema kwenye mitihani ya kitaifa na itabidi kila upande utimize jukumu lake la sivyo tutasalia kulaumiana huku na kule.

Hata hivyo, hatufai kukaa kimya wakati mambo yanapokwenda arijojo, elimu ya watoto wetu ni muhimu na tunafaa kufanya kila jitihada kuhakikisha haki yao ya kupata elimu inapewa kipaumbele.

Viongozi wetu wanafaa kuhakikisha kwamba misaada ya elimu almaarufu basari, inawaendea wanaostahili na wala haitolewi tu kwa wafuasi wao wa karibu huku wakiwafungia nje watoto mayatima na watoto kutoka familia maskini.

 

[email protected]