Habari Mseto

Mwongozo wa kuhudumia wagonjwa wa corona nyumbani

June 12th, 2020 2 min read

NA SARAH NANJALA

Wiki hii serikali ilitangaza kwamba wagonjwa wenye dalili chache ama hawana dalili zozote za corona wataruhusiwa kujitenga nyumbani na kupokea matibabu humo.

Kuna mikakati ambayo inapaswa kufuatwa ili kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo kwenye watu wa familia.

Hii ni moja ya miongozo inayopendekezwa kutumiwa wakati mtu anapokea matibabu nyumbani:

 • Kaa nyumbani na kuchunguza dalili. Unashauriwa usitoke nyumbani mara kwa mara isipokuwa pale una kitu cha maana cha kufanya kama kununua dawa ama mboga, kama inawezekana kuwa na mtu wa kutuma.
 • Jitenge na watu wa familia na marafiki. Kama inawezekana kuwa na chumba chako maalum, tumia bafu maalum na choo. Kama unatumia chumba kimoja na familia yako hakikisha kuna nafasi kati yenu, unaweza weka pazia.
 •  Hakikisha umevaa barakoa wakati wowote uko karibu na watu wa familia ama marafiki, hii itasaidia kutosambazia watu wengine ugonjwa,kumbuka kufunika mdomo na mapua na kitamba ama tishu unapokohoa ama unapopiga chafya.
 • Kaa ukijadiliana na daktari wako na maafisa wa afya ili kufuatilia jinsi unaendelea.

 

Ushauri kwa atakayehudumia mgonjwa wa corona:

 • Ni vizuri ajue dalili za corona ili aweze  kujua wakati mgonjwa anaendelea vizuri na kama anaendelea vibaya. Ujumbe huo unapatikana kwenye tovuti ya Shirika la Afya Duniani [WHO].
 • Unapaswa kusaidia mgonjwa kufuata maagizo ya daktari ya kukaa nyumbani na kunywa dawa. Hakuna dawa malum lakini dawa anazopewa mgonjwa ni za kupunguza makali ya dalili.
 • Hakikisha kwamba mgonjwa amekunywa maji mengi na kumsaidia katika kazi za nyumbani kama kupika, kuosha na ununuzi wa mboga.
 • Punguza kutangamana na mgonjwa. Mgonjwa awe na chumba chake maalum, vyombo vyake maalum.
 • Epuka wageni mpaka mgonjwa atakapopona.
 • Wakati unamshughulikia mgonjwa hakikisha umevaa glavu na barakoa. Hakikisha kwamba barakoa imefunika mafua na mdomo vizuri.
 • Fuatilia uzima wako wa mwili huku ukichunguza dalili kama joto mwilini na kukohoa.
 • Dalili za mgonjwa zikiendelea kuwa mbaya zaidi pigia daktari ama afisa wa afya simu.