MZAHA WA SONKO: Miguna akataa uteuzi

MZAHA WA SONKO: Miguna akataa uteuzi

Na WAANDISHI WETU

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko, alionekana kuwachezea shere wakazi wa Nairobi na taifa kwa jumla alipotangaza Jumatano usiku kuwa amemteua wakili mbishi Dkt Miguna Miguna kuwa naibu wake.

Hii ni kwa sababu alipotoa tangazo hilo, Gavana Sonko alifahamu uwezekano finyu wa Dkt Miguna kuwa naibu wake na hivyo tangazo hilo lilijitokeza tu kama mzaha ama lililokuwa na nia ya kuafikia malengo fulani ya kisiasa.

Kwa kufahamu tangazo lilikuwa la kuchezewa, Dkt Miguna alipuzilia mbali uteuzi huo akiutaja kama mbinu ya kumkanganya katika juhudi zake za kupigania kurudishiwa paspoti yake na vita vyake dhidi ya utawala anaosisitiza ni wa kidikteta.

Bw Sonko alifahamu kuwa hata kama Dkt Miguna angekubali uteuzi wa kuwa naibu wake jijini Nairobi, angekuwa ameanza safari isiyoelekea kokote. Kiti hicho kiliachwa wazi na Polycarp Igathe alipojiuzulu Februari.

Tatizo la kwanza ambalo Dkt Miguna angekumbana nalo ni kuwa kwa sasa Serikali inasisitiza hana uraia wa Kenya, ambao sharti awe nao ili kuhudumu katika wadhifa wa Naibu Gavana. Juhudi zake awali kutambuliwa kama raia zimegonga mwamba.

Bw Miguna, ambaye pia ana uraia wa Canada, alifukuzwa nchini Februari na alipojaribu kurejea mwezi uliofuata alikatazwa kuingia na badala yake akarudishwa Canada. Alikuwa amesema atakuja Kenya Jumatano lakini hakufanya hivyo kutokana na suala la paspoti yake.

Idara ya uhamiaji imesisitiza sharti Dkt Miguna afuate kanuni ili apate uraia wa Kenya ambao inasema aliukana alipochukua wa Canada kulingana na Katiba ya awali.

 

Uraia kwanza

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Beatrice Elachi alisema sharti wakili huyo angepata uraia wa Kenya kabla ya madiwani wa Nairobi kumpiga msasa kama inavyotakikana kisheria.

“Kwa sasa Dkt Miguna ni raia wa Canada. Ni sharti asuluhishe utata wa uraia wake na serikali,” alisema Bi Elachi.

Na iwapo Bw Miguna angeondolewa kizingiti cha uraia, angekabiliwa na kibarua kigumu cha kuwashawishi Bunge la Nairobi kuidhinisha uteuzi wake hasa ikizingatiwa Jubilee ina wingi wa wajumbe.

Alhamisi, Spika Elachi na Seneta Johnston Sakaja walipuzilia mbali uwezekano wa wakili huyo kuidhinishwa na bunge la kaunti. “Miguna hatakuwa Naibu Gavana wa Nairobi. Nawahakikishia hilo,” alisema Bw Sakaja.

Tatizo lingine ambalo angekumbana nalo ni kuwa yeye si mwanachama wa Jubilee. Kiongozi wa wengi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Abdi Guyo alisema jana kuwa wazo la Dkt Miguna kuwa Naibu Gavana ni ndoto tu.

 

Wanasiasa wa misimamo mikali

Suala lingine ni kuwa hata kama miujiza ingetendeka na ateuliwe, ingekuwa vigumu kwake kufanya kazi na Bw Sonko ikizingatiwa tofauti kali za misimamo baina yao.

Wawili hao wamekuwa wakirushiana cheche kali za maneno na kutofautiana vikali kuhusu uongozi wa Nairobi.

Mnamo Mei 2016, Bw Sonko alisema licha ya Dkt Miguna kumshambulia kila mara, atakapochaguliwa kuwa gavana atampa wadhifa katika serikali yake. Bw Miguna alijibu: “Ndugu yangu Sonko siwezi kuhudumu chini au pamoja na jambazi. Unaelewa?”

Wakati wa mdahalo wa wawaniaji wa ugavana Nairobi, Dkt Miguna aliwakabili vikali Bw Sonko na mtangulizi wake Dkt Evans Kidero kwa kile alichosema ni kushirikiana na wakora kufuja fedha za kaunti.

Kwa upande wake, Bw Sonko alimjibu Dkt Miguna kwa kumtaja kama ‘mtu mwenye akili punguani.’

You can share this post!

Kenya sasa nambari 111 duniani viwango vya soka

Pendekezo rais ahudumu kwa miaka 4 na seneta miaka 7

adminleo