Habari Mseto

Mzazi mwanamke afukuzwa shuleni kwa kuvaa long'i

February 4th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

MAAFISA wa Wizara ya Elimu katika Kaunti ya Vihiga wanachunguza kisa ambapo mzazi wa kike amelalamikia kuzuiliwa kuhudhuria mkutano katika shule iliyo eneo hilo kwa vile alikuwa amevaa long’i aina ya jeans.

Tukio hilo katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Goibei, limeibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii baada ya walinzi kumkataza Bi Jesca Awonda kuingia shuleni kwa sababu alikuwa amevaa suruali ndefu ya jeans.

Bi Awonmda alisema walinzi hao walimwambia aende abadilishe mavazi yake na kuvaa rinda au sketi ndipo akubaliwe kuhudhuria mkutano.

Mzazi huyo alikuwa amesafiri kutoka Nairobi hadi Vihiga mnamo Jumamosi kwa mkutano katika shule hiyo iliyoko eneobunge la Hamisi.

Lakini baada ya kupata mambo ambayo hakuyatarajia, hakuwa na budi ila kurudi hadi Nairobi bila kumwona dadake ambaye anajiandaa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) mwaka huu.

Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti hiyo, Bi Hellen Nyangau alisema uchunguzi unaendelea ili kubainisha kilichofanyika.

“Wakati nitakapopata ripoti kamili ndipo nitaweza kuzungumzia suala hilo. Kwa sasa niko Nairobi kwa shughuli za kikazi lakini nitarejea,” akasema Bi Nyangau.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Bessy Khabongo alikataa kuzungumza kuhusu suala hilo wakati tulipowasiliana naye.

Alisema anajiandaa kuarifu mkurugenzi wa elimu katika kaunti ndogo kuhusu kisa hicho.

Bi Awonda alisema aliwahi kwenda katika shule hiyo awali akiwa amevaa long’i na hakuzuiliwa kwa hivyo sheria hiyo mpya ilimshangaza.

MAAGIZO

“Mabawabu wawili waliniambia wana agizo kali kutoka kwa mwalimu mkuu wasiruhusu mzazi yeyote wa kike aingie akiwa amevaa long’i. Nilijaribu kuwaeleza kuwa sikupata mawasiliano yoyote kuhusu agizo hilo mapema lakini hawakutaka kunisikiza,” akasema Bi Awonda.

Alisema alisisitiza aongee na mwalimu mkuu ambaye alimwambia wazazi wanafaa kuheshimu sheria za shule kabla ya kuzuru.

“Nilimwambia anieleze kwa nini hapakuwa na mawasiliano kuhusu suala hilo lakini akasisitiza singeruhusiwa kuingia kama sitabadilisha mavazi nivae rinda au sketi,” akasema Bi Awonda.