Habari

Mzee, 83, apata makao mapya kijijini Nyamang'ara

March 6th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO
MZEE mmoja ambaye iliwahi kuripotiwa kwamba alitelekezwa na familia yake katika kijiji cha Nyamang’ara, Gatundu Kaskazini, amepata msaada na kujengewa nyumba mpya.
Bw Francis Kahura, 83, aliyekuwa akiishi msituni alipata afueni wakati mbunge wa eneo hilo Bi Anne Wanjiku Kibe, aliingilia kati na kumjengea nyumba mpya.
“Mimi nimeishi  msituni kwa muda mrefu baada ya jamaa zangu ‘kunitupa’,  huku wakikosa  kunitunza  ipasavyo. Sasa nina furaha kuu kuona ya kwamba Bi Kibe amenisaidia pakubwa,” alisema Bw Kahura mnamo Jumatatu huku akitabasamu.
Bi Kibe ambaye alizuru kujionea nyumba hiyo mpya iliyofunguliwa siku chache zilizopita alimkabidhi blanketi, godoro, na matandiko mengine muhimu kumsaidia mkongwe huyo  kujifunika vilivyo.
“Mimi furaha yangu ni kuona ya kwamba mkongwe huyu aliyetelekezwa na jamaa zake amerejea katika maisha mazuri. Nitahakikisha kila siku anakula vizuri na anatunzwa kwa njia inayostahili,” alisema Bi Kibe, na kuongeza, “Ningetaka nyinyi wakazi wa hapa pia muonyeshe moyo wa huruma kwa kumtunza mkongwe huyu ambaye mnamwona umri wake umesonga sana.
Ilidaiwa ya kwamba hapo awali mkongwe huyo alipokuwa msituni wahuni walimvamia na kumkata kwa panga ambapo alijeruhiwa vibaya, huku akipelekwa hospitalini.
Baada ya hapo ndipo ujumbe ulipowasilishwa kwa  mbunge wake Bi Kibe ambaye  bila kupoteza  muda aliamua  kumjengea nyumba ya chumba kimoja.
Makao maalumu
Wakazi wa kijiji hicho walimpongeza Bi Kibe kwa kuchukua hatua hiyo ya dharura na kuhakikisha mzee huyo mkongwe anapata makao maalumu.
“Sisi tumepongeza hatua uliyochukua ya kumhifadhi mkongwe huyu katika nyumba nzuri ya kisasa. Hiyo ni hatua  nzuri ya  kuonyesha jinsi unavyowatambua wasiojiweza, tunakushukuru zaidi,” alisema Paul Njuguna ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyamang’ara.
Familia za eneo hilo zimehimizwa kuwalinda wakongwe kwani hiyo ni baraka hata kwa Mwenyezi Mungu.
“Kila mara nitakuwa nikizuru eneo hili ili kumjulia hali mzee huyu ambaye ninamwita babu yangu na mzazi pia. Kwa hivyo  jukumu hili la kumchunga mzee wetu liwe letu sote na tutafanikiwa,” alisema Bi Kibe.