Dondoo

Mzee achekwa kumkasirikia kipusa aliyekataa mwanawe

May 21st, 2024 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

CHEBOLE, BOMET

BUDA wa hapa amekoma kumchangamkia kipusa wa hapa alipofahamu kuwa hawezi kuolewa na mwanawe.

Kulingana na duru, buda na kipusa ni washiriki wa kanisa moja eneo hili na mzee amekuwa akimsifu sana kipusa huyo akisema ana tabia njema.

“Mara kadhaa mzee amempa mrembo zawadi tele na kujipiga kifua kuwa ataolewa na mwanawe,” mdaku akaarifu.

Hata hivyo, mambo yalibadilika mzee alipofahamu kuwa mwanawe aliambulia patupu akimtongoza kipusa huyo.

Hapo ndipo buda huyo alianza kununa kila mara akikutana na mrembo huyo badala ya kujawa na bashasha na tabasamu kama hapo awali.

Juzi, wazee wenzake walimcheka kwa kuhamaki posa ya mwanawe ilipokatiliwa licha ya kujituma kwake kwa kutoa zawadi.