Habari za Kaunti

Mzee adai alisukumiwa kosa la unajisi kwa kudai deni

January 31st, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE 

MZEE mwenye umri wa miaka 78 anayetumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi msichana wa umri wa miaka minane anataka mahakama imuachilie huru kutokana na umri wake.

Isitoshe, kwenye rufaa, mzee Luke Owino anadai kuwa mama wa mtoto huyo alitumia mashtaka hayo ili kukwepa kulipa deni alilokuwa akimdai.

“Mama wa mtoto huyo aliniwekea utaratibu wa kushtakiwa baada ya kukataa ombi lake la kukopa bidhaa zaidi kwenye duka langu la mboga baada ya kushindwa kulipa deni la bidhaa alizochukua,” alisema Bw Owino.

Katika rufaa yake katika Mahakama Kuu mjini Eldoret, Bw Owino alidai kuwa mahakama ya chini ilikosea kumhukumu kifungo cha maisha jela.

Aliambia mahakama kwamba yeye ni mzee sana na kufungwa maisha gerezani kwa mashtaka ya ‘kuwekelewa’ ni sawa na kumuua kabla ya siku yake.

Kulingana na Bw Owino, mashtaka hayo yalipangwa ili kumzuia kudai malipo ya deni husika.

Alikuwa mfanyabiashara wa mboga ambapo anadai kuwa alikuwa amemuuzia mamake mtoto bidhaa kwa deni na alipotaka kulipwa, ndipo tofauti zao zilipoanza.

“Ukarimu wangu wa kukopesha jirani bidhaa umenifanya niozee gerezani katika umri huu ninapostahili kuwa nyumbani pamoja na wajukuu wangu,” aliambia Mahakama Luu ya Eldoret ambapo amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Aliomba mahakama imuachilie na iwapo mahakama haitaona umuhimu wowote katika rufaa yake, angependa apewe kifungo cha nje.

Mfungwa huyo aliiambia mahakama kuwa hata amekuwa mzigo gerezani ambapo anatakiwa kupewa uangalizi maalum kutokana na umri wake.

“Hata pale gerezani nimekuwa mzigo kwa askari wa gereza. Afisa mkuu wa gereza la Eldoret amekuwa akinionea huruma kwa kunipa kijana wa kunihudumia. Nimekuwa mzigo kwa gereza. Naomba mahakama hii iwapo ni lazima nihudumie kifungo, basi nipewe kifungo cha nje,” aliiambia mahakama.

Akiwa mbele ya Jaji Reuben Nyakundi, aliambia mahakama uamuzi wa kumfunga jela ni sawa na kupunguza miaka yake ya kuishi duniani kabla ya wakati Mungu Alikadiria maisha yake.

Rufaa hiyo itatajwa mnamo Machi 27, 2024, kwa maelekezo zaidi.