Habari za Kaunti

Mzee adaiwa kumuua mwanawe kwa mzozo wa pesa

February 1st, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMUME wa umri wa miaka 71 katika Kaunti ya Tharaka Nithi ametiwa mbaroni akidaiwa kumuua mtoto wake wa kiume wa umri wa miaka 28 kwa kumkata kichwani kwa upanga.

Kwa mujibu wa ripoti rasmi ya polisi wa kituo cha Magutuni kilichoko Kaunti ndogo ya Maara, wawili hao waligombana kuhusu pesa na ndipo hasira iliyotanda ikaishia mauti.

Kisa hicho cha usiku wa kuamkia Jumatano kimewaacha wenyeji kwa mshangao ambapo mzee huyo kwa jina Fabiano Kaburu Eugenio aliishia kukamatwa kama mshukiwa wa mauaji ya mwanaye.

Polisi walielezea kwamba shida ilianza kujiunda wakati Cliff Mwenda Kaburu akiwa amejihami kwa upanga alianza kudai pesa kutoka kwa babake.

“Lakini kuna ndugu yake ambaye kwa jina ni Maxwell Gitonga Kaburu wa miaka 38 ambaye aliingilia kati akiwa na nia ya kutatua mzozo huo. Lakini ndugu yake huyo aliyekuwa kwa mzozo na baba yao akamgeuka na akaanza kumkatakata kwa upanga,” ripoti hiyo ya Polisi yasema.

Shambulio hilo liliishia kumtwika nduguye majeraha ya shingoni, kifuani, miguumo na katika mikono.

Inadaiwa baba yao alimrukia kijana huyo na akampokonya upanga huo na kisha akamkata nao kichwani, hali ambayo ilisababisha kifo chake.

Wanakijiji walipiga ripoti kwa polisi ambao walifika katika eneo hilo na kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika mochari ya Chuka.

Naye majeruhi alipelekwa hadi hospitali ya Chuka ambapo Jumatano alikuwa mahututi.

[email protected]