Mzee aenda kortini kudai pesa kutoka kwa mwanawe

Mzee aenda kortini kudai pesa kutoka kwa mwanawe

Na GERALD BWISA

MZEE wa umri wa miaka 73 katika Kaunti ya Trans Nzoia ameitaka mahakama kushinikiza mwanawe wa miaka 48 kumgawia asilimia 20 ya mshahara wake wa kila mwezi.

Bw Gideon Kisira Cherowo, mkazi wa kijiji cha Birunda, eneobunge la Saboti, anasema alihangaika kumsomesha mwanawe, Washington Chepkombe Cherowo, hadi chuo kikuu lakini hajavuna matunda ya elimu ya mwanawe.

“Nilitumia mali yote niliyokuwa nayo kumwezesha mshtakiwa kupata elimu bora ili atusaidie katika siku za usoni. Lakini ningali naishi maisha ya umaskini ilhali mwanangu ameajiriwa. Ninaomba mahakama iagize niwe nikipewa asilimia 20 ya mshahara wake wa kila mwezi,” akasema Mzee Mzee Cherowo kupitia stakabadhi alizowasilisha kortini.

Mzee Cherowo anasema kuwa mwanawe anafanya kazi katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA) lakini hajafichua wadhifa anaoshikilia.

“Nimejaribu mara kadhaa tangu 2008 kutafuta msaada kwake bila mafanikio,” akasema Mzee Cherowo.

Mlalamishi anasema kuwa juhudi zake za kumsomesha mwanawe hazifai kuwa kazi bure.

Anasema kuwa aliuza ardhi yake katika eneo la Cheptais, Kaunti ya Bungoma kumsomesha mwanawe kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu.

“Vilevile, nilimpa robo ekari ya ardhi yangu na kumlipia mahari ya ng’ombe wanne na fedha,” akasema Mzee Cherowo.

Katika kesi hiyo, Mzee Cherowo hajawakilishwa na wakili yeyote bali anasema kuwa atapigania kesi yake mwenyewe.

Mzee Cherowo pamoja na mkewe wanaishi kwenye nyumba ya chumba kimoja katika katika eneo la Birunda, Saboti, Kaunti ya Trans Nzoia.

You can share this post!

Ronaldo aweka rekodi ya ufungaji mabao na kusaidia...

Ajipata kizimbani kwa madai ya kuiba nakala mbili za Biblia

T L