Michezo

Mzee aenziwa kwa kuvumisha soka miaka ya 80

February 5th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

WANAMICHEZO wanaendelea kuomboleza kufuatia kifo cha Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi aliyeaga dunia katika Nairobi Hospital.

Utawala wa Mzee Moi utakumbukwa kwa ujenzi wa uwanja wa Nyayo na ule wa Kimataifa wa MISC, Kasarani.

Uongozi wa klabu mbili kubwa nchini Gor Mahia na AFC Leopards, jana uliomboleza kifo cha Mzee Moi na kusema alichangia sana ufanisi ulioshuhudiwa miaka ya 80 na 90.

Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, alisema Mzee Moi alipenda mchezo wa soka na alitoa msaada wa kifedha kwa klabu hiyo kila mara iliposhiriki mechi za Bara Ulaya na ligi ya nyumbani.

Rachier pia alithibitisha kwamba Mzee Moi aliipa klabu hiyo vipande viwili vya ardhi katika maeneo ya Embakasi na Kasarani.

Mapenzi yake kwa K’Ogalo yalishuhudia akifika uwanjani na kutazama ngarambe ya fainali ya Kombe la Mandela ambayo Gor ilipiga Esperance ya Tunisia na kutwaa ushindi.

“Mzee Moi alipenda michezo na alifika uwanjani Gor Mahia ilipokuwa ikishiriki mashindano mbalimbali. Ingawa alitupa vipande vya ardhi, inasikitisha kwamba hadi leo hatujapata hatimiliki japo tunaendeleza mchakato wa kuhakikisha tunazipata kutoka kwa serikali,” akasema Rachier.

Mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda naye alisema walipewa ardhi na Mzee Moi na njia ya pekee ya kumuenzi kutokana na wema huo ni kuhakikisha wanapata hatimiliki ya ardhi hiyo iliyoko Kasarani.

“Natuma salamu za pole kwa familia ya Rais Mstaafu. Nilikuwa mchezaji alipotoa kipande hicho cha ardhi na najua mahali ipo. Kwa kuwa sasa mimi ni afisa wa klabu, nitajitahidi kuhakikisha tunapata hatimiliki ili kujenga pia uwanja wa mazoezi,” akasema Shikanda.

Aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee pia alikumbuka jinsi aliwaalika Ikulu waliposhinda Kombe la Cecafa mnamo 2000.

“Mzee Moi alitukaribisha kwenye ikulu tuliposhinda taji la Cecafa Kagame na lilikuwa tukio la kupendeza mno. Kwa masikitiko hatukupewa fedha zozote lakini naamini maafisa walioandamana nasi walituchezea shere na kuchukua pesa zetu. Hakuna vile ungeenda Ikulu kisha ukose kupokezwa kitita enzi hizo,” akasema Mulee.

Nahodha wa zamani wa Harambee Stars Musa Otieno pia alituma salamu za pole kwa familia ya Mzee Moi na kusema alikuwa akihudhuria mechi za timu ya taifa.