Dondoo

Mzee afurushwa basini kwa kutazama video za ngono

November 16th, 2018 1 min read

Na SAMUEL BAYA

Mtwapa, Mombasa

Mzee mmoja kutoka mtaa huu alilazimishwa kushukishwa kwenye matatu baada ya kupiga nduru akiangalia video za ngono kwenye simu.

Haikubainika mzee huyo ambaye alionekana nadhifu na mwenye hadhi alivyotekwa na uraibu huo, lakini abiria walisisitiza lazima ashuke.

Kulingana na mdokezi wetu, mzee huyo alipanda matatu katika kituo cha mabasi mjini Malindi akielekea Mombasa.

Akiwa kwenye matatu, aliendelea kujiburudisha pole pole huku akicheka na kutabasamu. Hakuna aliyedhani alikuwa akitazama picha chafu katika simu yake.

Kizaazaa kilizuka gari likikaribia kituo cha Mtwapa alipoanza kuongea na kupiga nduru.

“Ooh my God, yes, yes namna hii, yes hapo sawa,” alisema huku akionekana kama mtu aliyepagawa.

Ni hapo ndipo mama aliyeketi kando yake alipotupia jicho simu yake na akagundua kwamba mzee alikuwa akitazama picha za ngono lakini mara hii picha ilikuwa imemnogea.

“Wewe dereva. mshukishe huyu mzee. Anaangalia picha chafu. Wewe ni mtu mzima, sasa ni mambo gani ambayo unafanya hapa,” alifoka mama huyo.

Lakini jamaa ambaye alionekana kutotishika aliendelea kugandiza macho katika simu yake hadi pale kondakta alipomfikia na kumrai ashuke.

Lakini mzee huyo hakuwa tayari kushuka na akajitetea kwamba hakuwa ameudhi mtu yeyote.

“Mimi nimeingia gari hii huko Malindi na sijatatiza mtu yeyote. Yale ambayo nayafanya hapa nafanya kwa raha zangu. Kila mtu ana simu yake, aitumie,” alisema.

Hata hivyo matamshi yake yalizidi kuwaudhi mno abiria, hasa akina mama ambao walisema alikosa heshima na ingebidi ashuke.

Shinikizo za abiria zilimfanya dereva kusimamisha gari na mzee akashuka shingo upande.