Dondoo

Mzee akatazwa na wanawe kurudiana na mama yao

June 5th, 2024 1 min read

WERUGHA, TAITA

Na JANET KAVUNGA

MAMA mmoja hakuamini watoto wake walipomkataa kwa kuwaacha wakiwa wadogo na kurudi wakiwa watu wazima.

Inasemekana mwanadada huyo alimuacha mumewe na watoto wakiwa wa umri wa chini ya miaka mitano.

Baba yao aliwalea kwa shida hadi Chuo Kikuu. Hii ni baada ya juhudi za kumrai mkewe arudi kugonga mwamba. Mwanadada alihamia mjini Voi alikoishi maisha ya anasa hadi juzi hali ilipobadilika baada yake kuugua nusura atangulie kuzimu.

“Juzi alifika kwa boma la mumewe ambaye hakuoa tena ili kuwalea wanawe,”

“Alimpata mzee na wanawe waliokuwa wamemtembelea wikendi. Alipojitambulisha kwao kama mama yao, walikasirika na kumtaka arudi alikokuwa kwa miaka zaidi ya 24 walipokuwa wakimhitaji zaidi,” alieleza mdokezi.

Walimuonya baba yao dhidi ya kumkubali tena mama yao na kumwambia heri aoe mke mwingine wamwite mama kuliko huyo aliyewapuuza katika maisha yao ya utotoni.

“Hata kama mlikosana, angalau angeonyesha huruma kwetu lakini hakufanya hivyo,” alisema kitinda mimba kuunga mkono kakake aliyemtaka mama yao kutomsumbua baba yao katika maisha yake ya uzeeni.