Habari

Mzee jela miaka 30 kwa kunyakua kipande cha ardhi

November 21st, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

MAHAKAMA ya Embu, Alhamisi imemtoza faini ya Sh1.2 milioni Mzee Evanson Kihumba, 83, au atumikie kifungo cha miaka 30 jela kwa kunyakua kipande cha ardhi.

Mzee Kihumba anayeugua alisukunmwa jela kwa sababu alishindwa kulipa faini.

Hakimu Mwandamizi Samuel Mutai amemkuta mzee huyo na makosa sita ya kufanya hila kujipa kipande cha ardhi cha mmiliki aliyekuwa amefariki.

Hakimu Mutai alisema upande wa mashtaka kupitia mashahidi ulieleza bayana mshtakiwa alinyakuwa kipande hicho nambari Gaturi/Weru/377.

Ni makosa yaliyotekelezwa dhidi ya marehemu Nyaga Kombuthi mnamo Desemba 18, 1968, katika ofisi ya ardhi ya wilaya ya Embu ambapo mshtakiwa alisingizia kwamba aliinunua kutoka kwa Paul Kamara ambaye pia alishaiaga dunia.

Mashtaka mengine yalikuwa ni kughushi stakabadhi za kuhamisha umiliki kipande cha radhi, kutoa kiapo bandia Desemba 18, 2015, kwamba hatimiliki yake ya Gaturi/Weru/377 ilikuwa imeteketea na alitaka mpya.

Mzee Kihumba alikuwa ameshtakiwa na Bw Silas Muriithi kijana wa Kombuthi ambaye ndiye mmiliki halisi.

 

Hakimu alimtoza faini ya Sh200,000 kwa kila kosa au akae jela kwa miongo mitatu.

Wakili wa mshtakiwa Kirimi Guantai amesema atakata rufaa huku mkewe – Lucy – akielezea masikitiko.

“Sijafurahishwa na jinsi mambo yalivyokwenda, nadhani yanafaa kuangaliwa upya,” amesema Lucy.