Habari MsetoSiasa

Mzee Kenyatta alituchezea shere kuhusu mashamba, wasema Mau Mau

June 2nd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MANUSURA wa vita vya ukombozi wa taifa hili wamemtaka rais Uhuru Kenyatta awaelezee mashamba ambayo walikuwa watuzwe yalienda wapi.

“Tulimtuma hayati Mzee Jomo Kenyatta Uingereza katika uhai wake akatwae uhuru wa kujitawala na pia arejee akiwa na hatimiliki ya ardhi ya Kenya. Tukampa kauli mbiu ya Uhuru na mashamba iwe mwongozo wake wa kusukumana na wakoloni wa Uingereza. Aliporejea, jina mashamba lilikuwa limetoweka,” akasema Ngaruiya Kanyugo, mmoja wa manusura hao.

Wakiongea Mjini Murang’a huku maandalizi ya sherehe za makala ya 56 ya Madaraka Dei yakiendelea, Mzee Kanyugo alisema kuwa “Mzee Kenyatta alituhadaa na akaishia kutuchezea shere katika kuvuna manufaa halisi ya mapambano yetu na mabeberu.”

Alisema kuwa Mzee Kenyatta aliingizwa ‘boksi’ na wabeberu katika majadiliano yao ya kutuzwa Uhuru wa kujitawala “ambapo alikabidhiwa kidosho Mwingereza awe mkewe na aliporejea hapa Kenya, akatwambia Uhuru tushaupata, lakini akawa kimya kuhusu mashamba.”

Mzee kanyugo ambaye kwa sasa ako na miaka 92 aliteta kuwa “Mzee Kenyatta alijipa maekari ya mashamba yaliyo na rotuba kwanza, kisha akaanza kugawa mengine kwa vipimo kwa washirika wake wa karibu na pia kuwakubalia mabwanyenye wa kizungu kushikilia maelfu ya maekari ya mashamba.”

Akasema: “Kinyume na mwongozo wetu wa Maumau ambapo tulitaka usawa wa mwaafrika wa Kenya ajipe uwezo kamili wa kumiliki shamba na alitumie kwa manufaa yake nay a taifa hili, wengi wa wapiganiaji Uhuru waliambulia patupu.”

Aliteta kuwa hali hii imeendelezwa hadi serikali ya sasa “ambayo iko mikononi mwa motto wake hayati Kenyatta.”

Akasema: “Rais Kenyatta wa sasa ako na tabia ile ile ya babake ya kukatalia mwaafrika wa Kenya ajipe kipande cha ardhi kama haki yake ya uhuru. Tuko na wakimbizi wa ndani kambini na maskwota chungu nzima hapa Kenya miaka 56 baadaye.”

Alisema kuwa mtazamo wa rais Kenyatta ni kuwa “anayetaka kumiliki shamba ajinunulie yeye mwenyewe.”

Anasema kuwa yeye mwenyewe angejua mapema kuwa hali ingegeuka kuwa ya

Mkenya mwenye uwezo kumla Mkenya mwenzake asiye na uwezo, “singeshiriki kamwe vita hivyo vya ukombozi wa taifa hili.”

Alisema kuwa manusura wote wa mapambano hayo huaga dunia “wakiwa na msikitiko makuu ya kutapeliwa na kuhadaiwa na familia kubwakubwa zilizoishia kuvuna nafuu kutokana na uhuru wa taifa hili.”