Habari MsetoSiasa

Mzee Moi alazwa hospitalini Nairobi kwa matibabu

December 13th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

RAIS Mstaafu Daniel arap Moi, amelazwa tena hospitalini jijini Nairobi, afisi yake ilithibitisha Jumatano. 

Mzee Moi, 94, alilazwa katika Hospitali ya Nairobi Jumatano mchana ambako daktari wake, David Silverstein, alisema atakaa kwa muda usiojulikana ili kufanyiwa “uchunguzi wa kawaida wa kimatibabu.”

Mnamo Januari, rais huyo wa zamani aliyetawala Kenya kwa miaka 24 kuanzia 1978 hadi 2002, alifanyiwa upasuaji wa goti lake katika Hospitali ya Aga Khan University iliyo Nairobi.

Baadaye Machi, alisafirishwa hadi Tel Aviv, Israel, ambapo alilazwa hospitalini katika hali nyingine ambayo afisi yake ilitaja kuwa uchunguzi wa kimatibabu.

“Rais wa zamani atakaa hospitalini kwa siku kadhaa ili madaktari wapate muda wa kutosha kufanya uchunguzi wao,” ikasema taarifa kutoka kwa afisi yake.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua uchunguzi huo wa matibabu unahusu nini hasa.

Tangu aliporejea nchini kutoka Israel, Mzee Moi amekuwa akipokea wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Miongoni mwa viongozi ambao wamemtembelea mwaka huu ni Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

Ingawa viongozi hao husema wanaenda kumjulia hali, ziara hizo zimekuwa zikitazamwa kisiasa hasa ikizingatiwa kwamba mwanawe, Gideon Moi, ambaye ni Seneta wa Baringo, ameibuka kuwa hasimu mkubwa wa Naibu Rais William Ruto kisiasa katika eneo la Rift Valley huku siasa za 2022 zikipamba moto.

Juhudi za Bw Ruto kumtembelea Mzee Moi nyumbani kwake ziligonga mwamba alipomtembelea na kuzuiwa mlangoni kwa madai kwamba hakuarifu mapema kuhusu ziara yake akafika wakati ambapo rais huyo mstaafu alikuwa akihudumiwa na madaktari wake.

Rais Mstaafu Moi alianza kuugua goti lake mnamo 2006 baada ya kuhusika kwenye ajali wakati gari lake aina ya Range Rover lilipogongana na lingine la pick-up katika eneo la Rukuma, Limuru.