Habari MsetoSiasa

Mzee Moi alikula kiamsha kinywa cha ugali kwa mboga ughaibuni

February 10th, 2020 2 min read

Na MARY WAMBUI

MZEE Moi alikula ugali kwa mboga alipozuru mataifa ya kigeni. Aliposafiri aliandamana na wapishi wake kumwandalia mlo huo katika hoteli za kifahari kote duniani.

“Tulikula ugali katika hoteli ya Hilton ya jijini London, Uingereza. Nilimwona akila nyama na mboga kama kiamsha kinywa. Alikula mlo huo siku ambazo alifaa kuhudhuria vikao vilivyochukua muda mrefu,” Bw Frost Josiah, aliyekuwa mkuu wa itifaki wa Mzee Moi aliambia Taifa Leo Jumapili.

Rais wa pili wa Kenya aliyefariki Jumanne iliyopita akiwa na umri wa miaka 95, pia alivalia suti zilizoshonwa na fundi wa jijini London.

Mzee Moi hakunywa pombe wala kuvuta sigara. Lakini wakati wa hafla maalum: “Nilimwona akinywa angalau glasi moja ya mvinyo. Alipendelea mvinyo wa Black Tower na Spanish Rosily.”

Hakika, maisha ya kibinafsi ya Rais Moi yalikuwa siri kubwa kwa kipindi cha miaka 24 aliyoongoza nchi hii.

Miongoni mwa wandani wake ambao Mzee Moi aliamini alipokuwa kiongozi wa nchi ni aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Dkt Sally Kosgei na mawaziri Julius Sunkuli na Nicholas Biwott.

Bw Josiah anasema kuwa Moi alitunza wakati na alikuwa mchapa kazi. Aliamka saa kumi na mbili asubuhi na kuanza kuongoza mikutano saa moja asubuhi.

Bw Josiah ambaye sasa ni mkulima, anasema kuwa hakuna siku ambayo Rais Moi alikosa kuhudhuria kikao au hafla kwa kuwa mgonjwa.

Hata hivyo, Rais Moi alienda kufanyiwa uchunguzi na daktari kila alipozuru London. Mara nyingine alisafiri ughaibuni akiwa na daktari wake wa kibinafsi, Dkt David Silverstein.

Kulingana na Bw Josiah, Rais Moi hakuwa akifanya mazoezi lakini mwili wake ulikuwa imara.

Walinzi wake walihakikisha kuwa Rais Moi analala kwenye hoteli nzuri na Dkt Sally Kosgei aliidhinisha watu wote waliolala kwenye vyumba vyote vilivyokuwa karibu na rais.

Dkt Kosgei alihakikisha kuwa Mark Too anaandamana na Moi katika safari za ughaibuni kutokana na ucheshi wake. Too alimchekesha Moi hadi akatokwa na machozi.

Bw Josiah, ambaye ni mwana wa aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Bw Samuel Onyango Josiah, aliteuliwa kuwa mkuu wa itifaki wa Rais Moi mnamo 1997.

Kabla ya uteuzi huo, Bw Josiah, ambaye sasa ana umri wa miaka 70, alihudumu kama Balozi wa Kenya nchini Israeli.

Uteuzi wake kuwa mkuu wa itifaki ulipingwa na baadhi ya watu katika Ikulu kutokana na urefu wake.

Zamani, wadhifa huo ulipewa watu wafupi au waliolingana na rais kwa urefu.

“Nilipokea taarifa kuhusu uteuzi wangu kupitia arafa mnamo 1997. Lakini urefu wangu uliniweka pabaya na mlinzi wa Mzee Moi wakati huo, Kanali Alexander Sitienei, ambaye alikuwa akiniambia nimpishe. Mzee Moi alilazimika kuingilia kati kwa kumwambia: ‘wacha kijana afanye kazi yake.”

Walioabiri ndege moja na Rais Moi ni mkuu wa itifaki, mlinzi wa rais na mkuu wa mawasiliano wa kitengo cha rais, Bw Lee Njiru.

Maafisa wa serikali waliokuwa wakitarajiwa kukutana na Rais Moi walikwepa kunywa pombe au kuvuta sigara kwani hakutaka harufu ya vileo.

Bw Josiah anasema kuwa licha ya Moi kuwa na mamlaka makubwa, aliishi maisha ya upweke.

“Wakati ambapo marais wengine walikuwa wakisakata densi na wake au waume zao wakati wa hafla, Mzee Moi alicheza peke yake,” anasema Bw Josiah.