Habari MsetoSiasa

'Mzee Moi anaendelea vyema hospitalini'

November 14th, 2019 1 min read

Na ERIC MATARA

RAIS Mstaafu Daniel arap Moi anaendelea vyema na matibabu katika Hospitali ya Nairobi ambapo amelazwa.

Msemaji wake, Bw Lee Njiru Jumatano alisema Mzee Moi, 95, anatarajiwa kupata nafuu hivi karibuni ili aruhusiwe kurudi nyumbani.Alilazwa kwa mara nyingine Jumamosi, siku mbili tu baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.

“Anaendelea vyema na anatarajiwa kukaa hospitalini hadi wakati madaktari wake wakiongozwa na Dkt David Silverstein watakapomruhusu kuondoka,” akasema Bw Njiru.

Ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu ni lini Mzee Moi ataondoka hospitalini, alisema familia yake itatoa taarifa nyingine kesho kuhusu hali yake ya afya.

Kwa niaba ya familia ya Mzee Moi, msemaji huyo aliomba Wakenya na vyombo vya habari kujiepusha na uenezaji habari za kushtua kuhusu hali yake ya afya.

“Taarifa kuhusu afya yake zitatolewa kadri na jinsi inavyohitajika. Kwa sasa, Mzee Moi yuko thabiti na anaendelea kupokea matibabu kutoka kwa wataalamu wa kimatibabu wakiongozwa na daktari wake wa kibinafsi, Dkt David Silverstein,” akasema Bw Njiru.

Rais huyo wa zamani ambaye alilazwa hospitalini katika chumba cha watu mashuhuri alipelekwa huko mara ya kwanza Oktoba 12, ambapo familia yake ilisema alikuwa ameenda kwa ukaguzi wa kawaida wa kimatibabu.

Aliruhusiwa kuondoka hospitalini Alhamisi iliyopita baada ya kulazwa kwa wiki mbili, ikisemekana alikuwa akiugua maradhi ya kifua.

Mzee Moi alihitimisha umri wa miaka 95 mnamo Septemba 2, 2019.