HabariSiasa

Mzee Moi atazikwa Kabarak, familia yatangaza

February 4th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Mstaafu Daniel Arap Moi atazikwa nyumbani kwake Kabarak, eneobunge la Rongai, kaunti ya Nakuru, familia yake imetangaza.

Mzee Moi alizaliwa katika eneo la Sacho, Baringo ya Kati mnamo 1924 lakini akajenga makao katika shamba alilonunua Kabarak, alipokuwa akihudumu kama Makamu wa Rais miaka ya 1970s.

Ikiongozwa na mwanawe mkubwa Raymond Moi, familia hiyo imesema tarehe ya mazishi itatangazwa baadaye.

Raymond, ambaye ni Mbunge wa Rongai, amefafanua kuwa sasa masuala yote kuhusu kifo cha babake yataongozwa na wanajeshi na habari zote kuhusu mipango ya mazishi zitatolewa na msemaji wa Serikali Luteni Mstaafu Cyrus Oguna au afisa mwenye cheo cha juu serikalini.

“Ni takriban miezi mitatu tangu Mzee alipolazwa katika Nairobi Hospital. Tumehakikisha anatunzwa na kundi la madaktari kutoka nchini na mataifa ya ng’ambo lakini muumba wetu aliamua kinyume na matarajio yetu,” Raymond akasema kwenye kikao na wanahabari katika hospitali hiyo huku akiandamana na familia yake akiwemo Seneta Gideon Moi.

“Tunawashukuru wanajeshi na vikosi vingine vya usalama ambao wameingilia suala hili kwa haraka kwa kutoa misaada hitajika,” akaongeza.

Awali, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ambaye alifika katika hospitali hiyo akiandamana na Mkuu wa Majeshi Meja- Jenerali Samson Mwathethe alitangaza kuwa Kamati ya Kuandaa Mazishi ya Mzee Moi itaongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.