Habari MsetoSiasa

Mzee Moi kulipa Sh1 bilioni kwa kunyakua shamba la mjane

May 16th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HATIMAYE haki imetendeka kwa mjane aliyenyang’anywa shamba na rais mstaafu Daniel arap Moi zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu jijini Nairobi kumwamuru Bw Moi amlipe fidia ya Sh1 bilioni mjane huyo, Bi Susan Cheburet Chelungui na mwanawe David Chelungui.

Jaji Antony Ombwayo, aliyesikiza kesi hiyo, alisema Bw Moi alitumia mamlaka yake vibaya kutwaa shamba hilo mnamo 1983.

Jaji Ombwayo alisema mjane huyo aliporwa shamba lake kwa njia ya udanganyifu huku maafisa wakuu serikalini wakitumiwa kumpokonya shamba hilo.

Mahakama ilisema baada ya Bw Moi kusajiliwa kuwa mmiliki wa shamba hilo, aliliuzia kampuni ya Rai Plywood (K) Limited.

Shamba hilo, mahakama ilisema, mbeleni lilikuwa linamilikiwa na mlowezi Jacobus Hendrik EngelBrecht.

Hendrik aliuzia shamba hilo wanunuzi sita akiwemo marehemu Chelungui mnamo 1965. Kila mmoja wa wanunuzi hao sita alipata ekari 620.

“Ushahidi uliowasilishwa na mjane umethibitisha kuwa shamba la mumewe ndilo lililonyakuliwa na Bw Moi,” Jaji Ombwayo alisema.

Mahakama hiyo ilisema kuwa mbali na Bw Moi, sehemu ya shamba hilo iligawiwa aliyekuwa waziri msaidizi kwenye utawala wa Bw Moi, Bw Stanley Metto.

Shamba hilo limo katika Kaunti ya Uasin Gishu kwenye eneo lenye thamani kubwa.

Jaji Ombwayo alisema hakukuwa na ushahidi wowote kuonyesha uhalali wa rais huyo mstaafu kusajiliwa kama mmiliki wa shamba hilo.

Alisema Bw Moi alitumia vibaya mamlaka yake na mbinu zilizokiuka sheria, na hivyo mahakama haiwezi kulinda mali iliyopatikana kwa njia za udanganyifu.

Mahakama ilisema Bw Moi hakuwa kwenye orodha ya wamiliki sita asilia shamba hilo wa kampuni ya Langat and Partners, ambayo iligawa shamba hilo vipande sita miongoni mwa wanachama wake baada ya kuuziwa na Bw Hendrik.

Kwenye kesi hiyo, mlalamishi alishtaki Bw Moi, kampuni ya Rai Plywood, msajili wa mashamba Kaunti ya Uasin Gishu, msajili wa hati miliki za ardhi na Tume ya Ardhi.

Kesi hiyo ilianza kusikizwa mnamo 2014.