Habari Mseto

Mzee mwenye kidonda usoni atafuta usaidizi wa dharura

March 8th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 72 anahitaji msaada wa matibabu wa dharura baada ya kupata kidonda kisichopona haraka usoni.

Bw Joseph Karanja Kang’ethe, amejaribu kuzuru hospitali za aina nyingi lakini baada ya kufanyiwa ukaguzi na kupewa dawa za kutumia, bado hakuna jambo la kufurahia kwani kidonda kilicho usoni mwake kinaendelea kuenea kila kukicha.

Bw Kang’ethe anayetoka katika kijiji cha Gatuanyaga, Kaunti ya Kiambu, amebaki kusononeka asijue la kufanya baada ya kujaribu kuzuru hospitali mbalimbali; za kibinafsi na za umma.

“Janga hili lilinianza mwaka wa 1998 ambapo nilihisi kujikuna uso kila mara. Matokeo yake yakawa ni kidonda kinachoenea polepole. Sasa kimekuwa ni kidondo kisichoweza kupona kwa urahisi. Sijui nitakwenda wapi tena ili niweze kupata matibabu maalumu,” anasikitika Bw Kang’ethe.

Familia yake inasikitika.

“Sisi kama familia tumejaribu tuwezavyo kuona ya kwamba mzee anapata matibabu lakini baada ya kuzuru hospitali kadha bado hakuna cha kujivunia,” alisema mmoja wa jamaa zake ambaye hakutaka kutajwa jina.

Ala kwa shida

Bw Kang’ethe alisema tayari anahofia maisha yake yamo hatarini kwani maradhi hayo yanaendelea kuila sehemu ya uso wake ambapo hata kula chakula inakuwa ni kibarua kigumu kwake.

“Hata ninaona ya kwamba kidonda hicho kinaenea kwenye uso wangu sehemu ya kulia jambo linalokuwa tishio kwa meno yangu na macho kwa jumla,” alisema Bw Kang’ethe.

Alisema wakati fulani kidonda hicho huwa na usaha tele ambapo hata kujishughulikia inakuwa ni vigumu. Hata wanaojaribu kumsaidia wameonekana kupoteza imani naye.

“Imefika wakati kila mara nikizuru kwenye hospitali yoyote ninaambiwa tu niende nyumbani nijiuguze mwenyewe kwa vile hata wao wenyewe wamefika mwisho,” alisema Bw Kang’ethe na kuongeza, “Sisi kama familia tumejaribu tuwezavyo kutumia fedha zote tulizo nazo bila mafanikio.”

Anasema maradhi hayo yanayomfyonza hayaeleweki ambapo hata yeye ameshindwa la kufanya na yote amemwachia Mungu ambaye ndiye muweza yote.

Hapa kuna picha yake: Samahani sana kwa sababu tunaonyesha sehemu iliyo na kidonda.