Mzee na mwanawe wakamatwa kanisani wakivuta bangi

Mzee na mwanawe wakamatwa kanisani wakivuta bangi

Na Mwangi Muiruri

Mwanamume na mwanawe, walikamatwa Ijumaa usiku walipopatikana ndani ya kanisa moja Kaunti ya Murang’a wakivuta bangi huku wakiendelea kuisokota.

Simon Múthuri, 56, na mwanawe Julius Murigi, 19, walikamatwa ndani ya kanisa la Light of Hope Tabernacle Church mjini Mag wakitayarisha bangi hiyo kwenda kuuza.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Maragua Joshua Okello, wawili hao walikamatwa wakiwa na kilo 10 za bangi ambayo haikuwa imetayarishwa, misokoto 20 na vifurushi 41 vya dawa hiyo ya kulevya wanayodaiwa walitaka kwenda kuuza.

“Tulidokezewa kwamba wawili hao walikuwa na mazoea ya kuingia katika uwanja wa kanisa kujificha katika jengo linaloendelea kujengwa kupakia bangi wanayouza mjini Maragua. Tuliwavamia na kuwakamata,” alisema Bw Okello.

Mkuu wa kituo cha polisi cha Maragua Cleophas Juma alithibitisha kisa hicho na kusema wawili hao wanazuiliwaa seli za polisi wakisubiri kufikishwa kortini Jumatatu.

Bw Juma alisema viongozi wa kanisa hilo wamekuwa wakilalamikia kuvunjwa kwa jengo na kupata vipande vya bangi na sigara.

“Sasa tumejua wanaohusika na visa hivyo na watachukuliwa hatua za kisheria watakapofikishwa kortini Jumatatu,” alisema.

You can share this post!

BBI: Huenda juhudi za bunge zisizae matunda

Joho ajitokeza baada ya muda mrefu, aomboleza kifo cha BBI