Michezo

MZEE NI WEWE! Kipa Gianluigi Buffon atia saini mkataba mpya wa miaka mitatu Juventus

June 29th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

GOLIKIPA mkongwe wa Juventus, Gianluigi Buffon ametia saini mkataba mpya wa miaka mitatu na miamba hao wa soka ya Italia.

Mlinda-lango huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia atakayefikisha umri wa miaka 43 mkataba wake mpya utakapotamatika rasmi, alirejea Juventus mnamo 2019 baada ya kuhudumu kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa msimu mmoja.

Kufikia sasa, Buffon amechezea Juventus katika zaidi ya mechi 500 za ligi tangu aingie katika sajili rasmi ya kikosi hicho mnamo 2001. Alianza kusakata soka ya kulipwa kambini mwa Parma mnamo 1995.

“Super Gigi amethibitisha kwamba umri si hoja katika ulingo wa soka. Muhimu zaidi ni ari, moyo wa kujituma na msukumo wa ndani kwa ndani katika nafsi ya mtu,” ikasema sehemu ya taarifa ya Juventus.

Sogora mwingine ambaye amerefusha mkataba wake kambini mwa Juventus ni nahodha Giorgio Chiellini ambaye ametia saini kandarasi mpya ya mwaka mmoja.

Zikisalia mechi 10 pekee kabla ya kampeni za Serie A msimu huu kutamatika rasmi, Juventus wanaofukuzia ubingwa wa soka ya Italia kwa mara ya tisa mfululizo, wanadhibiti kilele cha jedwali la Serie A kwa alama 69.