Dondoo

Mzee wa kanisa mpenda uroda afichuliwa

December 10th, 2019 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

KAVIANI, MACHAKOS

MZEE mmoja wa kanisa eneo hili alipata aibu ya mwaka alipoandikia demu mmoja wa kanisa hilo arafa ya kimahaba na siri ikafichuka kanisani humo.

Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, mzee huyo alishurutika kujiuzulu kutoka kwa kamati ya kanisa na pia akaacha kuhudhuria ibada zote kwa sababu ya kugubikwa na aibu,

Mzee huyo alikuwa mshauri mkuu kanisani. Aliheshimiwa mno na kuenziwa na kila mja kanisani humo. Kwa ufupi, alikuwa kipenzi cha watu wengi,” asema mpambe wetu.

Tuliarifiwa kwamba, mzee huyo wa kanisa alikuwa akiandaa hafla tofauti katika makongamano mbalimbali ili kuwapa vijana ushauri-nasaha. Alikuwa akiwahimiza vijana wawe Wakristo wa kweli na kujiepusha na mienendo na tabia inayoweza kuathiri maisha yao ya siku za usoni.

“Ni lazima vijana muwe waadilifu. Jiepusheni kabisa na visa vinavyoweza kuathiri maisha yenu ya baadaye. Kumbatieni neno la Bwana kikamilifu, na bila shaka mtaona matunda na mafanikio yake,” polo alikuwa akiwashauri vijana.

Inasemekana kwamba, mzee huyo alikuwa chui aliyevalia ngozi ya kondoo. Alikuwa akimtamani demu mmoja kanisani humo.

Siku ya tukio, buda aliamua liwe liwalo na akaamua kuandikia demu huyo jumbe fupi za kimapenzi akimuarifu alikuwa akimfeel sana awe mtu wake.

“Darling, unionavyo, nakumiss sana. Umbo lako, sauti yako mwanana na mienendo yako zimenibamba mno. Hakika, naomba tuwe wapenzi wa dhati, yaani wa kufa kuzikana,” polo aliandikia demu huyo arafa.

Duru zaarifu kuwa, demu huyo alikasirika mno kutokana na ujumbe huo , tena kutoka kwa mzee wa umri wa babake na akaamua kumfundisha adabu.

“Demu alienda katika mkutano wa wanakamati baada ya ibada na akalalamika kusumbuliwa na buda huyo. Aliwaonyesha wanakamati ‘sms’ alizokuwa akimwandikia na wote wakabaki vinywa wazi” asema mdaku wetu.

Kulingana na mdokezi, buda aliingiwa na kiwewe na akajiuzulu kutoka kwa kamati. Alikoma pia kuhudhuria ibada kanisani humo.