Michezo

Mzee Wenger akataa kuinoa Fulham

November 14th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

ALIYEKUWA kocha wa Arsenal Arsene Wenger ameripotiwa kukataa kazi ya ukufunzi wa klabu ya Fulham ambayo ilipandishwa ngazi msimu huu wa 2018/19 na wakaishia kumkabidhi kocha wa zamani wa Leicester Claudio Ranieri kazi hiyo.

Kulingana na Jarida la kispoti la Mirror, Fulham waliitisha huduma za Wenger walipokuwa wakimtafuta kocha ila akakataa na ikabidi wameze machungu na kumkumbatia Ranieri.baada ya kumfuta kocha wao wa zamani Slavisa Jokanovic.

Mfaransa huyo amewahi kunukuliwa akisema kwamba hatainoa timu yoyote inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) kama njia ya heshima kwa waajiri wake wa zamani Arsenal.

Habari hizo zinajiri majuma machache tu baada ya taarifa kuibuka Wenger aliwapa shingo mabingwa watetezi wa klabu bingwa barani Uropa Real Madrid ambao pia walimfuta kazi aliyekuwa kocha wao Julen Lopetegui.

Akiwa Arsenal, kati ya mwaka wa 1996 na 2018,  Wenger alishinda mataji matatu ya ligi, saba za kombe la FA na saba za Kombe la ngao ya jamii ambalo hukutanisha mshindi wa FA na bingwa wa EPL kwenye mechi ya kufungua msimu.

Claudio Ranieri anakumbukwa kwa kuongoza Leicester kutwaa ubingwa wa EPL mwaka wa 2016.