Habari Mseto

Mzigo wa deni la nchi sasa wavuka Sh4.5 trilioni

March 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mzigo mkubwa wa deni la serikali utazidi kuandama Wakenya katika muda wa miaka mingi ijayo baada ya deni la jumla kuvuka Sh4.5 trilioni.

Kwa mara ya kwanza, deni la umma limevuka kiwango hicho na kufikia Sh4.57 trilioni kulingana na ripoti ya utafiti wa Hazina ya Kitaifa ya Fedha kufikia Desemba 2017.

Kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka zaidi kabla ya mwisho wa mwaka huu kwani serikali imeonekana kuendelea kukopa, nje na ndani ya nchi.

Hii ni licha ya serikali kuonywa na mashirika ya kimataifa na wataalam dhidi ya kukopa zaidi.

Mwaka wa 2016 Desemba, kiwango hicho kilikuwa Sh3.82 trilioni. Kulingana na ripoti hiyo kulikuwa na ongezeko la Sh746.7 bilioni zilizokopwa katika muda wa mwaka mmoja.

Mikopo kutoka nje ya nchi ni asilimia 51.9 ilhali mikopo kutoka nchini ni asilimia 48.1.

Hapo Februari, serikali ilikopa Sh210 bilioni kupitia utoaji wa Eurobond.