Habari Mseto

Mzozo IEBC ni njama ya kuiba kura 2022 – ANC

April 19th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

CHAMA cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, kimedai mzozo unaokumba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni njama ya kupanga wizi wa kura ifikapo mwaka wa 2022.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Barrack Muluka (pichani), Alhamisi alisema mzozo huo uliopelekea makamishna watatu kujiuzulu mapema wiki hii unachochewa na watu ambao walisababisha uchaguzi uliopita kuwa usioaminika.

“Tunataka wajue tutapinga juhudi zozote za kunyakuwa mamlaka ya urais kupitia kwa uchaguzi mwingine mbovu wa urais utakaosimamiwa na IEBC isiyoaminika na yenye ubaguzi,” akasema kwenye taarifa kwa vyumba vya habari.

Naibu Mwenyekiti wa IEBC, Bi Consolata Maina, alijiuzulu Jumatatu pamoja na makamishna, Bi Margaret Mwachanya, na Dkt Paul Kurgat. Hali hii imesababisha tume kusalia na makamishna watatu pekee ambao ni Mwenyekiti, Bw Wafula Chebukati, na makamishna Boya Molu na Prof Abdi Guliye.

Kamishna Roselyn Akombe, alijiuzulu mwaka uliopita kabla uchaguzi wa marudio wa urais uliofanywa Oktoba 26, akidai haingewezekana kusimamia uchaguzi huru na wa haki wakati tume ilikuwa imegawanyika kisiasa na kulikuwa na vitisho dhidi ya maafisa wa IEBC.

Kwenye taarifa yake, Bw Muluka pia alidai kuna watu wanaotaka kushawishi matokeo endapo kura ya maamuzi itaitishwa kufuatia makubaliano kati ya serikali na upinzani, na matokeo ya utathmini upya wa maeneo ya mipaka nchini ambao unatarajiwa kuanza kuandaliwa hivi karibuni.

Sawa na Chama cha ODM, katibu huyo alisema ANC inataka pia afisi ya usimamizi inayosimamiwa na Bw Ezra Chiloba, aliyesimamishwa kazi kwa muda, iondolewe na maafisa wachunguzwe kwa ukiukaji wa sheria ili walio na hatia wachukuliwe hatua za kisheria.