Habari Mseto

Mzozo Kebs ikizuia bidhaa za Coca-Cola bandarini

November 2nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mgogoro umeibuka kati ya kampuni ya Coca-Cola na Mamlaka ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs) kwa sababu ya bidhaa za thamani ya Sh500 milioni zilizozuiliwa bandarini Mombasa.

Hii ni kutokana na operesheni inayoendelea kuhusiana na bidhaa ghushi nchini. Mkurugenzi Mkuu wa Coca-Cola Beverages Africa (CCBA) Daryl Wilson alisema bidhaa hizo ambazo ni sukari nyeupe na resini zimekuwa bandarini tangu Julai, hali ambayo imefanya kampuni hiyo kupata hasara ya Sh100 milioni, gharama iliyotokana na bidhaa hizo kuendelea kukaa bandarini humo.

Alisema baadhi ya bidhaa zake zilizozuiliwa zina uwezo wa kuharibika jinsi zinavyoendelea kukaa humo.

Kebs na Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) zilitoa notisi Mei kwa waagizaji wote wa bidhaa za kusafirishwa kupitia majini au hewani kusajili na mamlaka hizo ili bidhaa zao ziweze kukaguliwa kwa kutumia kanuni mpya zilizoundwa 2005.

Serikali imekuwa ikafanya kampeni kubwa kukabiliana na bidhaa ghushi nchini kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita.