Habari Mseto

Mzozo kuhusu Ken Okoth kurejea mahakamani

August 3rd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEJITOKEZA akisema ni mpenziwe marehemu Mbunge wa Kibra Ken Okoth, Anne Muthoni Thumbi, ametisha kushtaki familia ya mwendazake Jumatatu kwa kutomshirikisha mwanawe katika hafla fupi ya kuteketeza mwili wa marehemu Jumamosi.

Wakili Elkanah Mogaka, ameikashifu familia ya Okoth kwa kukaidi makubaliano waliotia saini mahakamani Ijumaa kwamba Bw Thumbi na mwanawe watashirikishwa katika maandalizi ya hafla ya kumpumzisha.

“Hafla ya uteketezaji mwili iliofanyika katika tanuri ya Kariokor ilifanyika kisiri bila kuhusisha mteja wangu na mwanawe, kulingana na makubaliano yaliyoafikiwa Ijumaa. Hii ndio maana taarifa iliwekwa katika ukurasa wa akaunti yake ya Twitter,” akasema Jumamosi.

Wakili Mogaka alisema mnamo Ijumaa familia ya Mbunge huyo, kupitia wakili Edwin Sifuna, walikubali mahakamani kushirikisha Bi Thumbi na mwanawe katika shughuli zote za kumpumzisha Okoth.

“Ningependa kuwahakikishia kuwa Jayden hakushirikishwa katika sherehe ya uteketezaji na ilivyo ni kwamba familia ilidharau agizo la mahakama na hivyo tutashughulikia suala hilo Jumatatu,” Bw Mogaka akawaambia wanahabari.

Lakini Bw Sifuna alisema hafla hiyo ilikuwa ni shughuli ya kibinafsi na kwamba Bi Thumbi, ambaye ni diwani maalumu katika Bunge la Kaunti ya Nairobi aliamua kutoshiriki.

“Sherehe hiyo ilianza alfajiri mbele ya watu wachache pekee. Wakili wa Anne alisema jana (Ijumaa) kwamba hawangehudhuria,” akasema Bw Sifuna.

Mnamo Ijumaa, mahakama moja ya Nairobi iliidhinisha makubaliano yaliyotiwa saini na mjane wa Okoth, Monica Okoth na Bi Anne Thumbi ambapo wawili hao walikubaliana kwamba uchunguzi wa DNA ufanywe kubaini babake mtoto.

Wawili hao pia walikubaliana kwamba mtoto angehusishwa kushiriki katika mipango ya kumpumzisha maiti ya Okoth.

Hii ni baada ya Bi Thumbi kwenda mahakamani akitaka mazishi ya mpenziwe yasitishwe hadi utata kuhusu asili ya mtoto ubainishwe.

Alitaka mtoto huyo mvulana mwenye umri wa miaka mitano atambuliwe kama mwanawe Okoth.