Mzozo kuhusu mpaka watesa watoto shuleni

Mzozo kuhusu mpaka watesa watoto shuleni

NA MAUREEN ONGALA

WANAFUNZI wa shule ya msingi ya Bengoni iliyo katika Wadi ya Mwanamwinga, Kaunti ya Kilifi, wanalazimika kutumia mabanda kama madarasa kwa vile kuna utata kuhusu eneobunge ambapo shule hiyo imejengwa.

Viongozi wa kisiasa katika eneobunge la Ganze na Kaloleni wamekuwa wakitofautiana kuhusu upande ambapo shule hiyo iko, na hivyo kukataa kufanya ukarabati na ujenzi unaotakikana katika shule hiyo.

Wakati mwingine, wanafunzi huwa wanalazimika kusomea chini ya miti wakikalia magogo na mawe.

Kulingana na Diwani wa Mwanamwinga, Bw Edward Ziro, shule hiyo ilijengwa na shirika lisilo la kiserikali na ikasajiliwa katika Wadi ya Bamba, eneobunge la Ganze.

Shule hiyo ilianzishwa katika mwaka wa 2010 ikasajiliwa mwaka wa 2016.

Usajili wake katika Wadi ya Bamba badala ya Mwanamwinga, ndio ulikuwa chanzo cha mizozo kuhusu eneobunge linalofaa kuhudumia shule hiyo.

“Hali hii imeleta uatata na changamoto kwa miaka mingi kwa sababu mbunge wa Kaloleni hangeweza kuwekeza fedha na kuendeleza shule ambayo iko katika eneo bunge la Ganze. Vilevile, wabunge wa Ganze walisusia kuwekeza kwani inafahamika iko katika eneobunge la Kaloleni,” akasema Bw Ziro.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi shule hiyo mabati 100 kwa ujenzi wa madarasa, Bw Ziro alisema ataandaa kikao kati ya viongozi na wabunge kutoka eneobunge la Kaloleni na Ganze kusulihisha utata huo kwa manufaa ya watoto na jamii.

Shule ya msingi ya Bengoni ina zaidi ya wanafunzi 500 na madarasa matatu tu.

Ukosefu wa madarasa ya kutosha imewalazimu kugawanya hayo matatu mara mbili-mbili.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw Franklin Chiruu, alisema kuwa walichukuwa darasa moja katika yay ale matatu na kufanya afisi ya walimu hatua ambayo imepingwa vikali na shirika hilo lilojenga madarasa hayo.

Bw Chiruu alisema walichukua darasa moja la chekechea kuwapa wanafunzi wa darasa la kwanza lakini hatua hiyo ikapingwa na Serikali ya Kaunti ya Kilifi.

Vilevile, walimu hawana afisi yoyote na huwa wanakaa nje kupanga kazi zao.

“Hii imekuwa changamoto kubwa kwetu lakini kama shule tunawaomba viongozi wetu waweze kushikana kusaidia shule ya Bengoni kwa sababu wakiangalia mambo ya siasa, anayeumia ni mtoto,” akasema.

Kibanda hicho kinatumika na wanafunzi wa Gredi ya 2 na 3 ambao hupishana kupata mafunzo.

Bi Safari alisema kuwa kibanda hicho imekuwa hatari kwa wanafunzi hao kwani wameponea maisha mara kadhaa wakati kinataka kuanguka kwa sababu ya upepo.

 

Mmoja wa walimu katika shule ya msingi ya Bengoni katika mpaka wa eneo bunge la Kaloleni na Ganze kaunti ya Kilifi juzi akiwafunza wanafunzi chini ya mti. Tangi la maji limegeuzwa kuwa ukuta wa kuandikia. PICHA | MAUREEN ONGALA

Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi wa shule hiyo, Bw Stephen Matoo, alisema shule hiyo iko katika eneo la ukame na haistahili kutengwa kwa sababu ya siasa.

“Mara kwa mara tunakosa maji. Na tunapoendelea kusubiri msaada wa maji, watoto nao hawaji shuleni kwa sababu ya njaa na ukosefu wa maji,” akasema.

Mmoja wa walimu, Bi Rebbecca Safari, alisema ukosefu wa madarasa ya kutosha uliwalazimu kujenga kibanda cha mabati.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti ya Mombasa yalenga kuvuna zaidi kwa makongamano

MCAs wapandisha joto la kudai nyongeza ya malipo

T L