Habari Mseto

Mzozo kuhusu umiliki wa vipande vya ardhi wazidi kushuhudiwa Thika

November 2nd, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANANCHI wengi mjini Thika, wanazidi kulalamika jinsi wanavyoendelea kuchengwa kuhusu utoaji wa vyeti vya ununuzi wa ardhi.

Naibu kamishna wa Thika Magharibi, Bw Mbogo Mathioya, alisema tayari amepata malalamiko kwamba eneo lililo na shida zaidi ni mtaa wa Kisii mjini Thika.

Akizungumza kwa njia ya simu mnamo Ijumaa wiki jana alitoa wito kwa watu walio na shida ya ardhi wapige ripoti mara moja katika afisi ya ardhi mjini Thika ili kufanywe uchunguzi.

“Tayari watu wengi wamefika katika afisi yangu wakieleza jinsi wawalivyochengwa kwa kupewa hatimiliki zilizo ghushi huku kipande kimoja cha ardhi kikiuziwa zaidi ya watu wawili,” alisema Bw Mathioya.

Alisema watafanya kikao na afisi ya ardhi ili kupata njia mwafaka ya kukabiliana na jambo hilo.

Alisema kuna mpango wa kuleta maafisa wa ardhi kutoka Nairobi ili kuhamasisha wakazi wa Thika kuhusu haki yao.

Mkazi wa kijiji cha Kisii mjini Thika Bi Joyce Wanjiku alisema alinunua kipande cha ardhi katika eneo hilo mwaka wa 2013 ambapo alianza kujenga nyumba yake hapo.

“Hata hivyo hivi majuzi kuna watu walikuja na kuniambia eti walinunua ardhi hiyo. Sasa nimeshindwa kuelewa kinachoendelea,” alisema Bi Wanjiku.

Alisema watu walionunua ardhi mahali hapo wameteseka pakubwa kwa sababu kuna watu wengine wanaokuja eti pia wamenunua ardhi mahali hapo.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Bw Humphrey Irungu alisema alinunua kipande cha ardhi miaka sita iliyopita na hadi wa leo hajapata cheti maalum kuhusiana na ardhi hiyo.

Alisema watu wengi wakijaribu kujenga nyumba katika maeneo hayo zinabomolewa na wahuni wakisema pia wamenunua sehemu hizo.

“Tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi kujitokeza wazi ili kusaidia watu walioathirika kutokana na ulaghai huo unaoendelea maeneo hayo,” alisema Bw Irungu.

Bw John Kimani ambaye wamekuwa mahali hapo kwa zaidi ya miaka minane anasema bado hawajapokea cheti cha kumiliki ardhi hiyo.

“Kwa hivyo tunaomba afisi ya ardhi, machifu, naibu kamishna, na maafisa wa upelelezi waingilie kati ili kutafuta ukweli wa mambo,” alisema Bw Kimani.

Alisema jambo hilo linastahili kufuatiliwa haraka iwezekanavyo bila kuchelewa kwa sababu watu wengi wamekuwa na wasiwasi.

Bw James Butali alisema karibu mara mbili amekuwa akipata vitisho huku akiambiwa ahame mahali pale.

“Ningetaka serikali kuingilia kati ili kutuokoa kabla ya mambo kuharibika. Mimi nimetishwa mara mbili eti nihame nitoke pahala pangu,” alisema Bw Butali.