Habari MsetoSiasa

Mzozo ndani ya Jubilee ni hatari kwa muafaka, mashirika yaonya

January 8th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

MASHIRIKA mbalimbali yameonya kuwa mizozo ya Chama cha Jubilee inahatarisha mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa kutokana na muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

Mwafaka huo wa Machi 9, umekuwa ukisifiwa na wengi kuleta utulivu wa kisiasa kwa kiwango cha kutoa mandhari bora ya kibiashara.

Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda (KNCCI) kimesema siasa za urithi wa 2022 na kura ya maamuzi zinaweza kuathiri ukuaji wa uchumi.

Kulingana na Mweneyekiti wa Kitaifa wa chama hicho, Bw Kiprono Kittony, biashara nyingi zingali zinatatizika kurejelea hali ya kawaida baada ya kuathirika wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2017 na hivyo basi ni muhimu utulivu udumishwe.

“Tunaomba wanasiasa waepuke kampeni za mapema tunazoshuhudia. Bado ni mapema mno kuruhusu siasa za urithi kuteka midahalo yetu ya kitaifa,” akasema, kwenye taarifa.

Aliongeza: “Tutumieni 2019 na 2020 kujenga uchumi wetu na kuleta umoja wa nchi kupitia kwa mipango tofauti kama vile hadnsheki.”

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Mwenyekiti wa kitaifa wa baraza hilo, Bw Stephen Cheboi, alikosoa wanaoingiza siasa kwenye mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga na kuwataka watazame mwafaka huo kama njia ya kusaidia wananchi.

Alizidi kuambia viongozi wajiepushe na kutusi wenzao hadharani.

Mvutano katika Chama cha Jubilee umezidi kushuhudiwa wiki hii kufuatia malumbano kati ya Rais Kenyatta na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanaodai amepuuza eneo hilo kimaendeleo licha ya kumwezesha kushinda urais mara mbili mfululizo.

Jubilee pia kinakumbwa na misukosuko baada ya aliyekuwa Naibu Mwenyekiti, Bw David Murathe, kudai hapakuwa na maelewano yoyote kwamba Naibu Rais William Ruto ataungwa mkono kuwania urais na jamii ya Wakikuyu ifikapo mwaka wa 2022.