Habari Mseto

Mzozo polisi kuhusu ni kikosi kipi kinase magari ya makaa

October 4th, 2019 1 min read

Na BONIFACE MWANIKI

MZOZO umeibuka kati ya vitengo vya idara ya polisi katika Kaunti Ndogo ya Mumoni, Kitui, kuhusu utekelezaji wa agizo la kunasa malori yanayosafirisha makaa kutoka Tseikuru-Katse hadi eneo la Irira.

Ripoti zasema mzozo huo unahusu ni kitengo kipi kinapaswa kuyakamata malori hayo yanayoshiriki kwenye biashara hiyo ya mamilioni ya pesa. Inasemekana polisi huwa wanapewa pesa nyingi kama mlungula na wafanyabiashara hao.

Mzozo huo ulidhihirika wazi Jumatano usiku baada ya gari moja lililokuwa likisafirisha makaa kutoka Mbuga ya Wanyama ya Kora kuelekea Tseikuru lilipokamatwa katika eneo la Iria, kwenye mpaka kati ya kaunti za Kitui na Tharaka Nithi.

Maafisa wa polisi kutoka Kitengo cha Ulinzi wa Miundomsingi (CIPU) wa kilichokuwa kikosi cha polisi wa utawala na wale wa kawaida walizozania lori hilo lililokamatwa, ambapo nusura wafyatuliane risasi.

Marufuku

Mwaka 2018 Gavana Charity Ngilu alipiga marufuku usafirishaji wa makaa katika kaunti hiyo, hali iliyoungwa mkono na serikali ya kitaifa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku uchomaji makaa na ukataji mbao katika misitu yote ya serikali. Bi Ngilu aliapa kukomesha uharibifu wa mazingira kupitia uchomaji makaa ambao ulikuwa ukiendelea katika kaunti hiyo hata kabla yake kuchukua uongozi.

Hata hivyo, hatua hiyo haikuwafurahisha baadhi ya watu.

Kulingana na Naibu Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Mumoni Bw Samuel Kogo, maafisa wa polisi kutoka kitengo cha CIPU walikiuka majukumu yao kwa kuweka kizuizi cha barabarani usiku huo.

Alisema walikuwa wakisindikiza lori hilo lenye nambari ya usajili KBX 166, lililokuwa likisafirisha makaa kutoka Tseikuru hadi Irira bila stakabadhi zifaazo.

“Tulipata ripoti kuwa gari la polisi hao lilikuwa likisindikiza lori lililokuwa limebeba makaa likielekea eneo la Irira. Ni kwa sababu hiyo ambapo niliwaagiza maafisa wangu kuhakikisha lori hilo halipiti mpaka kuingia katika Kaunti ya Tharaka Nithi bila ufahamu wao,” akasema mkuu huyo.