Kimataifa

Mzozo wa Kenya na Tanzania waathiri biashara mpakani

July 22nd, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

WAFANYABIASHARA katika soko la mpakani la Taveta, Kaunti ya Taita Taveta wameitaka serikali kuingilia kati mzozo wa kibiashara kati yao na nchi ya Tanzania.

Wafanyabiashara hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilalamikia kusumbuliwa na maafisa wa mipaka wa Tanzania, walisema kuwa nchi hiyo jirani haijatilia maanani mchakato wa soko huru ulioletwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Walisema kuwa licha ya kuwa serikali ya Kenya imewaruhusu wafanyabiashara wa nchi ya Tanzania kuuza bidhaa zao nchini, hali ni tofauti kwa Wakenya kufanya hivyo katika soko za nchi hiyo.

Wakiongea mjini Taveta, baadhi yao walidai kukamatwa na kisha bidhaa zao kuchukuliwa na maafisa wa mipakani.

Soko la Taveta lililopo mpakani limeshuhudia ongezeko la raia wa nchi hiyo jirani wanaoingia kuuza bidhaa zao bila pingamizi.

“Sisi hatuwezi kupeleka bidhaa zetu hata katika soko za mji jirani wa hapa Holili. Ukifika mpakani mizigo inachukuliwa ama wakati mwingine unatozwa ada za juu,” akasema mfanyabiashara mmoja, Bw John Mutua. Walisema kuwa muungano wa nchi za Afrika Mashariki huenda ukakosa maana kwa Wakenya ikiwa nchi zingine zinajivuta kutekeleza makubaliano ya jumuiya hiyo.

“Sisi Wakenya tunaumia sana. Ukifaulu kupeleka mzigo huko wafanyabiashara wa hapo wanakukataza kuuza. Hii jumuiya haina maana kwetu,” akasema mfanyabiashara mwingine, Bi Grace Mwanyika.

Hata hivyo, wafanyabiashara kutoka nchi ya Tanzania walieleza kuwa wanafanya shughuli zao kwa amani kwa kuwa serikali ya Kenya imewaruhusu kufanya biashara huru.

“Hatujapata shida yoyote huku. Tunauza bidhaa zetu kila siku ya soko na jioni tunarudi nyumbani,” akasema Bi Lisa Ngimwa. Bidhaa kadha wa kadha zikiwemo zile za shambani, vinywaji, sabuni, vyombo vya nyumbani na simu kutoka nchi hiyo hufurika katika soko hiyo kila Jumatano na Jumamosi.

Wanunuzi hupendelea bidhaa za nchi hiyo kwa kuwa bei yake ni rahisi zikilinganishwa na zile za huku nchini.