Habari za Kaunti

Mzozo wa kipande cha nyama wasababisha vifo vya ndugu wawili

May 14th, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

MWANAMUME wa umri wa miaka 57 ambaye inadaiwa alimuua kakake Ijumaa wiki jana wakizozania nyama na kisha kutorokea katika shamba la miwa, ameuawa na umma wenye ghadhabu kijijini Papaa, Teso Kaskazini.

James Ocharo anadaiwa kumuua kaka yake mdogo, Gracio Ogulo walipotofautiana namna ya kugawana nyama ya ini la ng’ombe katika mazishi ya jamaa yao.

Wawili hao walizua ugomvi ambao uliishia kifo cha Ogulo.

Inadaiwa baada ya Ocharo kutekeleza unyama huo alitoroka kutoka eneo la tukio.

Inadaiwa alimdunga kakake tumboni kwa kisu baada ya kushindwa kuafikiana ni nani kati yao angebeba ini, nyama inayopendwa mno.

Ogulo alifariki papo hapo huku mshukiwa akitoroka.

Hata hivyo, Ocharo alipatikana Jumatatu akiwa amejificha katika shamba la miwa lililo karibu huku akiwa na silaha hatari ikiwemo panga.

Waliokuwa wa kwanza kumuona mafichoni walisema alikuwa anatishia kila mtu karibu naye kuwa angemuua yeyote ambaye angethubutu kumkaribia.

“Alitutishiai kwa nia ya kuua lakini tulifaulu kutoroka na kuwaarifu majirani wengine ambao walikuja wakiwa wamejawa ghadhabu,” alisema Bw Joseph Ojuma, ambaye ni mwanakijiji.

Msako mkali ulianzishwa na wanakijiji ambao walimtafuta mshukiwa kila kona ya shamba hilo na Jumatatu jioni, walifanikiwa kumpata.

“Wanakijiji wenye hasira walianza kumpiga kwa mawe huku wengine wakimshambulia na kumrushia kila aina ya vifaa butu na mapanga. Ilikuwa ni hatari pale,” alisema Bw Benson Ojaka, ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Papaa.

Alisema marehemu amekuwa tishio kwa usalama eneo hilo baada ya kudaiwa kumuua kaka yake.

Kamanda wa polisi kaunti ya Busia Bw Ahmed Abdille alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo viwili na kuwashutumu wananchi kwa kujichukulia sheria mkononi.

“Haikuwa sawa kwa wanakijiji kumuua mshukiwa. Walifaa kuripoti kisa hicho kwa polisi ili hatua ifaayo ichukuliwe. Tunachunguza suala hilo na tunatumai kuwakamata waliohusika na mauaji hayo,” akasema Bw Abdille.