Habari za Kitaifa

Mzozo wa uongozi wa Supkem wachacha

January 28th, 2024 1 min read

NA KNA

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) tawi la Garissa limekashifu Msajili wa Vyama vya Kijamii na Dini kwa kusababisha mzozo unaozingira baraza hilo kuhusu nani anastahili kushikilia wadhifa wa mwenyekiti.

Msajili wa Vyama vya Kijamii na Dini mnamo Januari 23, 2024 aliandika barua ya kumrejesha Yusuf Abdulrahman Nzibo kama mwenyekiti wa Supkem kwa mujibu wa rekodi za 2017.

Hata hivyo, Bw Nzibo aliondolewa na Baraza Kuu la Supkem (NEC) mnamo 2019 na akaelekea kortini ambapo msajili huyo huyo alithibitisha kuwa Bw Naado ndiye mshikilizi wa wadhifa wa mwenyekiti.

Viongozi hao wa kidini walisema kuwa Septemba 2024, msajili alishangaza kwa kurejesha kundi la Bw Nzibo na kufanya uongozi wa sasa urejee mamlakani.

Walipata amri ya kumzuia msajili dhidi ya kuvuruga uongozi wa Supkem.

Jumapili, Januari 28, 2024, viongozi wa Supkem kutoka Garissa wakiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji Deghow Iman walisema wao wanamuunga mkono Bw Ole Naado.

“Uongozi halali wa Supkem ni ule ambao unaongozwa na Hassan Ole Naado. Ni baraza kuu pekee ndilo lina wajibu kutoa uamuzi kuhusu uongozi wa Supkem,” akasema Bw Iman.

“Msajili wa vyama vya kijamii na dini amefeli mara nyingi tu kutekeleza wajibu wake kulingana na sheria. Mizozo inayohusisha mashirika ya kidini inastahili kushughulikiwa kwa njia ya heshima na kwa kufuata sheria,” akaongeza.

Viongozi hao sasa wametoa wito kwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi aingilie suala hilo na amshauri msajili akome kuingilia masuala ya Supkem kwa kutoa amri ambazo zinavuruga uongozi wake.

Mnamo Ijumaa, Bw Nzibo akiwa ameandamana na baadhi ya waumini, alijaribu kuingia katika afisi za Supkem katikati mwa jiji lakini akapata lango limefungwa.

Bw Nzibo alikuwa ameandamana na baadhi ya akina mama ambao walibeba mabango ya kumtaka Bw Ole Naado aondoke afisini huku wakidai amekuwa akiongoza baraza hilo vibaya.