Habari za Kitaifa

Mzozo wa urithi wa maduka ya Naivas wachacha

February 4th, 2024 1 min read

Na JOSEPH OPENDA

MZOZO kuhusu usimamizi wa mali ya mwanzilishi wa maduka ya Naivas Peter Mukuha unaendelea baada ya watoto wake watatu kutaka kuchukua nafasi ya kaka yao kama msimamizi.

Newton Kagira Mukuha, dadake Grace Wamboi na kaka yake David Kimani Mukuha wamewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Nakuru wakitaka kuteuliwa wasimamizi wa mali ya thamani ya mabilioni badala ya kaka yao Simon Gashwe aliyefariki Agosti 2019.

Bw Gashwe aliteuliwa kuwa msimamizi wa mali hiyo 2016 kabla ya uamuzi huo kupingwa na Bw Kagira, rufaa ambayo bado haijaamuliwa na mahakama.

Katika ombi lake lililowasilishwa 2022, Bw Kagira anadai anahofia kwamba mali hiyo itaharibiwa kwa kukosa uwakilishi na kuongeza kuwa huenda ikaporwa na wageni.

Kulingana naye, kifo cha Gashwe ni sababu tosha ya kubatilisha msimamizi na kuteua mpya.

Alidai ugavi wa mali ya Mukuha ulikuwa haujakamilika hadi wakati wa kifo cha Gashwe mnamo 2019.

David Kimani kwa upande mwingine anadai nduguze ambao ni Teresia Njeri, Charles Mukuha Gashwe, Grace Muthoni Mukuha, Ruth Wanjiru Mukuha, Hannah Njeri Mukuha na Linet Wairimu Mukuha wamekubali awe msimamizi.

Alisena hakuna mrithi yeyote wa Bw Gashwe ambaye amekubali kuteuliwa kwa Kagira na Wamboi kuwa wasimamizi.