Habari za Kitaifa

Mzozo watokota shule ya kifahari ya Mang’u High baina ya mwalimu na wazazi

May 1st, 2024 2 min read

NA DAVID MUCHUNGUH

MVUTANO unatokota katika shule ya kitaifa ya Mang’u High kati ya mwalimu mkuu na wazazi wanaomtuhumu kwa kuongeza karo kiholela na kuendesha hoteli ya kibinafsi shuleni miongoni mwa tuhuma nyingine.

Kulingana na stakabadhi ambazo Taifa Leo imeziona, mwenyekiti wa Muungano wa Wazazi shuleni humo, Bw Benson Mwenje, amewasilisha kesi kortini kutaka mwalimu mkuu John Kuria achukuliwe hatua za kisheria.

Bw Mwenje anataka Bodi ya Elimu katika Kaunti ya Kiambu na Wizara ya Elimu ichunguze suala hilo.

Hakimu Mkuu wa Thika Oscar Wanyaga ametoa amri ya muda dhidi ya nyongeza ya karo ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka Sh33, 750 hadi Sh37,615.

Kulingana na nyaraka za korti, Bw Mwenje anadai kuwa Bw Kuria alijenga hoteli mwaka 2024 na ambayo anaendesha mwenyewe shuleni akiuzia wanafunzi vyakula vya starehe ambavyo si sawa katika shule za umma.

“Hoteli hii imefanya wazazi wakapokea malalamishi kuwa baadhi ya wanafunzi wanawafulia wenzao nguo ili waweze kupata pesa za kuwawezesha kumudu vyakula vya bei ghali. Hoteli hii imetenganisha wanafunzi kitabaka. Wanafunzi wanatumia wakati mwingi hotelini humo, hali inayofanya wazazi kuingiwa na hofu,” nyaraka za korti zinasema.

Mlalamishi amedai kuna maswali kuhusu madai ya ubadhirifu wa fedha shuleni.

Vile vile ameeleza kuwa muungano wa wazazi uliagizwa kushiriki mkutano ulionuiwa kumwondoa mwenyekiti wa muungano wa wazazi kwa kile anachosema ni kushinikiza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa shule.

Kesi hiyo itatajwa Mei 7, 2024, ambapo siku ya kusikilizwa itaratibiwa.

Katika barua iliyotumwa kwa afisi ya elimu katika kaunti, mwenyekiti wa muungano wa wazazi alidai kuwa mwalimu mkuu anafaa kustaafu mwishoni mwa mwaka huu na akaomba halmashauri kuingilia kati masuala yanayohusu shule hiyo.

Bw Mwenje alifika kwa Hakimu Mkuu kwa mara ya kwanza mnamo Aprili 2, 2024, akitaka aamuru kusitishwa kwa mkutano shuleni siku iliyofuata.

Ijapokuwa Hakimu Mkuu Stella Atambo alitoa maagizo ya muda jinsi alivyotaka mlalamishi, mkutano uliendelea.

Bw Kuria aliandika barua kwa wazazi wote kuonyesha Bw John Kanyoni alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa muungano wa wazazi.

“Mkahawa wa shule huendeshwa kulingana na kanuni za shule. Uboreshaji wa hoteli ama nini kinafaa kuuzwa ama kutouzwa huamuliwa na mjadala kati ya kamati ya muungano wa wazazi na ile ya miundomsingi ya shule,” akasema mwalimu mkuu.

Alijitetea kuwa shule hiyo ilituma vitabu vya uhasibu kwa mkaguzi mkuu wa fedha na kuwa kila kitu kiko sawa.

Katika barua kwa Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Bw Mwenje anadai kuwa mkuu wa shule alisajili wanafunzi 1,164 wa kidato cha kwanza mwaka wa 2024 kinyume cha uwezo wa shule.

Barua hiyo pia imepokelewa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) na Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Serikali.

Bw Kuria anatuhumiwa “kutoza sehemu ya wazazi wa kidato cha kwanza (600 – 700) Sh25,000 zaidi ya karo iliyoidhinishwa na zililipwa kupitia akaunti haramu ya kupokea hela.

Madai yameibuka kuwa ada hizo hazikudhinishwa na bodi ya usimamizi, wazazi au serikali.

Vilevile, Bw Mwenje amewasilisha kesi kortini kutaka mwalimu mkuu ashtakiwe kwa kukiuka amri ya mahakama kwa kusimamia mkutano mnamo Aprili 3, 2023, kinyume cha sheria.

TAFSIRI NA LABAAN SHABAAN